Ni huyu Manji mnayemzungumzia?

Mwandishi Wetu

Yusuf Manji
NI Yusuf Manji anayezungumziwa? Hilo ni swali analoweza kujiuliza mtu yeyote anayemfahamu mfanyabiashara huyo kwa haiba yake na matendo anapozunguzmiwa na kumhusishan na mambo yaliyo kinyume katika jamii.

Muda mfupi baada ya kutajwa kuhusishwa na dawa za kulevya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Manji ameeleza kushtushwa na kitendo hicho, hata kuhoji kama ndiye anayezungumziwa.

Katika mahiojiano na gazeti hili Manji alifananisha kutajwa kwake kwenye tuhuma hizo kuwa ni sawa na mti wenye matunda kupigwa mawe.

Alisema kuwa licha ya kuunga mkono vita ya dawa za kulevya, utaratibu uliotumika kumtaja haukubaliki na umemchafua katika jamii aliyoihudumia kwa muda mrefu

“Nimejitoa kwa mambo mengi kuhakikisha Watanzania wenzangu wanapiga hatua kaitka maendeleo, ajira, elimu, afya hata michezo na siasa,” alisema.

Alisema jina lake ni miongoni mwa Watanzania maarufu nchini waliojitoa kwa jamii kupitia mambo mbalimbali, jina la Yusuf Manji halitowekwa kando.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba Manji (42) amekuwa akijitoa na kujitolea katika masuala mbalimbali kiuchumi na kijamii hata kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia Kampuni ya Quality Group Limited (QGL) anayoiongoza.

Manji amekuwa akiongoza QGL yenye biashara takriban 102 katika nchi 28 duniani tangu akiwa na umri wa miaka 20.

 Alipata uongozi huo mwaka 1995, baada ya baba yake Mehboob Manji kufariki dunia. Mzee Mehboob alikuwa akiendesha kampuni ya vifaa vya magari.

Tangu wakati huo, Manji amekuwa akisimamia vyema na kupata mafanikio yaliyowezesha kuongeza kampuni 17 tangu alipoanza kuongoza kampuni hiyo ameweza kuajiri mamia ya Watanzania kwenye fani mbalimbali hivyo kuchangia kuboresha maisha ya Watanzania kwa kipato na pia ukuaji uchumi wa Taifa.

Kampuni hizo zinajihusisha na biashara ya kimataifa, huduma za vyakula, usambazaji vyombo vya moto, maendeleo ya makazi na huduma za uchukuzi.

Mfanyabiashara huyo anetekeleza hayo kukiwa na faida kadhaa za uwekezaji wa ndani kwa taifa.

Moja ya faida hizo ni kupunguza tatizo la ajira kwa wananchi, kuongezeka kwa bidhaa na huduma bora kwa wananchi, lakini kubwa fedha na faida za uwekezaji kubaki nchini.

Tayari Serikali ya Awamu ya Tano chini ya RAIS John Magufuli imeeleza kujipanga kuwasaidia na kuwaunga mkono wawekezaji wote wa ndani, ikiwahakikishia ulinzi wa viwanda vyao.

Katika moja ya mikutano yake na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kwa ajili ya utoaji wa Tuzo za Rais kwa wazalishaji bora nchini, Rais Magufuli ameshamwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha anatengeneza mazingira yatakayowapunguzia kodi kwa kiasi kikubwa wawekezaji wa ndani na kupandisha kodi zaidi kwa bidhaa zinazoingia kutoka nje ya nchi.

Alisema Tanzania ni nchi yenye utajiri wa rasilimali, fursa ya masoko, nguvukazi na mazingira mazuri ya uwekezaji, hivyo kipaumbele kikubwa kitakuwa ni kuhakikisha wazalendo wanapata fursa ya kufungua viwanda kwa wingi na kutumia ipasavyo fursa hiyo.

Alitaja faida watakazopata wafanyabiashara wa Tanzania endapo watawekeza na kuanzisha viwanda nchini kuwa ni pamoja na kuongezea Taifa mapato, kuingiza zaidi fedha za nje na kutengeneza ajira kwa wingi.

Rais aliwataka Watanzania hasa watendaji Serikali na taasisi zake, kuondokana na tabia ya wivu kwa kuwanyima fursa wawekezaji wa ndani wanapotaka kuwekeza, badala ya kuwapendelea na kuwaamini zaidi wawekezaji kutoka nje.

Pamoja na maelezo hayo kwa haiba, Manji amejipambanua kama mpenda watu hasa vijana kwa kujihusisha na michezo akiwa Mwenyekiti wa Klabu Kongwe ya Yanga na amekuwa akijitolea kiasi kikubwa cha fedha kuiendesha.

Mbali na masuala ya michezo, Manji ni mwanasiasa na Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, Dar es Salaam, nafasi aliyoipata katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2015.

Kupitia wadhifa huo, amekuwa akihudumia wananchi wa kata hiyo katika nyanja tofauti ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa wote kwani lengo la kugombea nafasi hiyo kwake lilikuwa kuhudumia wakazi hao hasa kuhakikisha wanapata huduma bora.

Manji ameboresha huduma za afya kwa wakazi hao kwa kujenga hospitali kwenye kata hiyo ya Mbagala Kuu, kuboresha upatikanaji wa elimu.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa QG Ltd pia ameanzisha Mpango wa Kutoa Uji kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za kata hiyo hali inayohamasisha watoto kupenda shule lakini pia kuwa na afya bora.

Mara kadhaa katika mahojiano na vyombo tofauti vya habari Manji amejipambanua kwamba nia yake ni kuona Tanzania inasonga mbele na watu wake wanapata maisha bora.

Aliwahi kueleza kuwa akimaliza kipindi chake cha udiwani nafasi anayotamani kuiwania ni ujumbe wa nyumba kumi ili kuwatumikia wananchi wa kawaida.

Pia aliwahi kueleza kwamba ikiwa ataombwa kuwania ubunge, basi atakuwa tayari kufanya hivyo katika majibo yenye umasikini mkubwa ili kusaidia kuondoa hali hiyo kwa Watanzania.

Anatajwa kama mmoja wa Watanzania wenye mafanikio akiwa miongoni mwa matajiri 10 nchini hali ambayo binafsi amekuwa akiielezea ni matunda ya juhudi na kujituma, huku akisema yeye si tajiri bali ni mtumishi katika QG Ltd kama walivyo wengine.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 comments:

Laptop City

Tangazo