Sababu 10 vyuo vikuu nchini kupoteza sifa


Suleiman Msuya

Ukumbi wa Nkrumah
WAHADHIRI wametaja zaidi ya sababu 10 zinazochangia vyuo vikuu nchini kukosa sifa za kuingia kwenye ubora wa vyuo Afrika Mashariki, Afrika na Duniani, huku kutofanya utafiti kukitajwa kama sababu kuu.

Sababu hizo zimetajwa siku chache baada ya Taasisi ya Webometrics ambayo inajihusisha na kupanga ubora wa vyuo vikuu kutaja vyuo bora 100 Afrika huku Tanzania ikiingiza vyuo vitatu kwenye 10 bora.

Akizungumza na JAMBOLEO jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa, alizitaja sababu hizo kuwa ni ukosefu wa utafiti, idadi ya wanafunzi, walimu wenye Shahada ya Uzamivu na maprofesa, kutobadilishana wahadhiri na wanafunzi kutoka nje.

Dk Mkonongwa alisema sababu nyingine ni sifa za wanafunzi wanaodahiliwa na programu ambazo zinafundishwa kuwa za kimataifa.

“Chuo kikuu ni taasisi za kimataifa, hivyo ili uweze kuingia kwenye ushindani, mambo mengi huangaliwa hasa utafiti, jambo ambalo kwa wahadhiri wa Tanzania halifanyiki kutokana na kutumia muda mwingi kufundisha na kusahihisha mitihani,” alisema.

Mhadhiri huyo alisema wahadhiri wengi wa Tanzania wanafundisha zaidi ya wanafunzi 2,000 jambo ambalo linasababisha washindwe kutumia muda mwingi kufanya kazi za kijamii.

Alisema wakati Tanzania ikikabiliwa na mazingira hayo, katika vyuo vilivyondelea hali ni tofauti ambapo mwalimu anaweza kufundisha wanafunzi wasiozidi 200, hivyo kutumia muda mwingi kuandika machapisho ya kitafiti.

Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere (MNMA), Dk Thomas Ndaluko alisema pamoja na changamoto zingine, anaamini miundombinu, machapisho kidogo na mafunzo adimu kwa walimu ni sababu mojawapo.

Dk Ndaluko alisema ili kuingia kwenye ubora wa kidunia na Afrika, ni kazi ambayo inachukua muda mrefu hasa katika nchi ambazo hazijawekeza kwenye elimu ipasavyo.

“Si jambo la siku moja, ndiyo maana sisi hapa MNMA tumeamua kuruhusu walimu takribani 50 waende kusoma uzamivu, ili kuwa na watu sahihi katika sekta hiyo,” alisema.

Alisema kwa sasa wana mkakati wa kubadilishana wahadhiri na vyuo vitatu vya nje, huku wakijiandaa kupokea wanafunzi kutoka nje.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe (MU), Lusekelo Kwasongwa alisema vigezo vinavyutumiwa ni vingi, huku akibainisha kigezo kimojawapo kuwa ni maktaba za kutosha na walimu bora kitaaluma.

Kasongwa alisema vyuo vingi nchini vina uhaba wa walimu hasa wenye sifa ya uzamivu, hivyo ni vigumu kuingia kwenye ushindani wa taasisi hiyo.

Alisema pia vyuo vingi havijihusishi na utafiti hiyo ikichangiwa na changamoto za kifedha hivyo kuwa vigumu kuwa miongoni mwa  vyuo bora Afrika au Afrika Mashariki.

Katika ripoti hiyo, Chuo Kikuu cha Rwanda kilikuwa kikiongoza kwa ubora siku hadi siku ambapo kati vyuo 26,300 Afrika ikiwa na vyuo 1,520 chuo hicho kilifanikiwa kuwa katika 100 bora kwa kushika nafasi ya 96 kutoka 123 Julai mwaka jana.  

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Chuo hicho mwaka huu kimeshika nafasi ya 3,499 kutoka ya 3,907.

“Chuo hiki kimefanya vizuri kwani kimeingia 10 Bora ya EA kutoka nafasi ya 11 mwaka jana ila pia katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara kiko nafasi ya 52 kutoka 67 ya mwaka jana,” ilisema taarifa.

Ripoti hiyo ilisema Januari mwaka jana, chuo hicho kilikuwa cha 140 Afrika na 72 Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hali kadhalika taarifa hiyo inaonesha kuwa katika Afrika Mashariki Chuo Kikuu cha Nairobi, ndicho kinaongoza kikishika nafasi ya nane Afrika kikifuatiwa na Makerere cha Uganda ambacho kwa Afrika ni cha 11.

Vingine kwenye 10 bora ni Kenyatta, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jomo Kenyatta, cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na cha Teknolojia cha Jomo Kenyatta, Mbarara cha Uganda, Chuo Kikuu cha Afya, Sayansi ya Tiba Muhimbili (MIHAS) na Egerton cha Kenya.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo