Watakiwa kujiunga kwenye vikundi


Mwandishi Wetu

WAKULIMA wadogo katika mikoa 10 wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kupata kuwezeshwa kubadili mfumo wa maisha kupiti kilimo.

Katibu Mtendaji wa Mfuko Kichochezi wa Kuendeleza Kilimo Biashara Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, Dk. John Kyaruzi alisema Dar es Salaam jana kuwa kuna fursa nyingi kwa wakulima wadogo wanaojiunga katika vikundi.

Dk. Kyaruzi alisema, ili kubadili mfumo wa kilimo na kuwa cha biashara lazima kuwepo na mazao ya kutosha ambayo yana ubora, miundombinu mizuri ikiwemo barabara na upatikanaji wa maji ya uhakika kwa mwaka mzima.

“Mkulima mdogo ana changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa mtaji, mbolea, dawa za kuua wadudu shambani, mbinu bora za kuhifadhi mazao kabla ya kuyauza, vifaa bora vya kisasa pamoja na uhakika wa soko. Yote haya yapo chini ya uwezo wetu, tunachotaka wakulima wajiunge na wapeleke malalamiko yao kwa kampuni au taasisi moja ambayo tutaitumia kutatua matatizo yao.

Akitoa mfano alisema wakulima wa miwa Morogoro au Kagera, wakilalamika ubovu wa barabara watazungumza na Kiwanda cha Sukari Mtibwa au Kagera Sugar watengeneze hizo barabara kisha wawape mchanganuo na kuwalipa, au wakulima wakilalamika ukosefu wa pembejeo watazungumza na kampuni inayosambaza pembejeo itoe huduma hiyo kisha wao ndio hulipa gharama zote.

“Tunachotaka ni kumaliza changamoto zinazomfanya mkulima ashindwe kutoa mazao bora na mengi, kwa kawaida soko linataka kitu kilicho bora kwa idadi kubwa. Kiwanda cha nyanya kinaweza kuhitaji tani 1000 kwa siku, lakini wakulima katika mkoa husika uwezo wao ni kulima nusu yake lazima mwekezaji ataagiza bidhaa hiyo nje ya nchi, sisi tunataka kuondoa hilo,” alisema DK. Kyaruzi.

Akizungumzia matatizo ya kukopesha wakulima alisema, huo si uamuzi sahihi kwa sababu kumkopesha maana yake ni kumfunga mkulima asiwe huru kwa kile anachofanya akifikiria namna ya kurudisha fedha alizokopa.

“Wakulima wadogo wana matatizo mengi ya kifedha, mkopo hauwezi kuwa suluhisho la matatizo yao zaidi ya kuongeza matatizo, unaweza kumpa mkopo mkulima akaanza kutatua matatizo ya nyumbani ikiwemo afya au sare za shule za mtoto wake, hadi akianza kulima fedha yote ameimaliza kwenye matatizo ya kifamilia, tukasema mbinu hii si muafaka,” alisema Dk. Kyaruzi.

Kwa sasa mfuko huo unasaidia wakulima katika mikoa 10 ambayo ni Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Dodoma, Singida, Rukwa, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya na Rukwa, ambapo mfuko huo wa kuchochea kilimo unalenga ongezeko la viwanda maeneo hayo kulingana na aina ya mazao yanayolimwa ikiwemo matunda, mbogamboga, nafaka na mifugo.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo