Watanzania 132 watimuliwa Msumbiji


Emeresiana Athanas

Dk Susan Kolimba
WATANZANIA 132 wamekamatwa na kufukuzwa nchini Msumbiji wakituhumiwa kuishi bila kufuata taratibu za uhamiaji.

Watanzania hao wamekamatwa mjini Monte Puez jimboni Cabo Delgado kwenye operesheni maalumu ya kuwakamata na kuwarudisha kwao raia wa kigeni wanaoishi nchini humo kinyume cha taratibu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Susan Kolimba, alisema kutokana na tukio hilo ubalozi wa Tanzania nchini humo umefika eneo hilo kufuatilia na kujionea hali halisi.

"Sisi si kwamba tunapingana na mchakato huo, lakini tunafuatilia ili kujua kama raia hao wanatendewa haki na wanatolewa kihalali kwani tumepata malalamiko kwamba wapo walionyang'anywa pasipoti zao na kunyanyaswa," alisema.

Alisema ubalozi unaendelea kufanya mawasiliano ya kidiplomasia na Serikali ya Msumbiji ili kuhakikisha usalama wa Watanzania na mali zao na kinachofuata kuwahusu.

"Kuna baadhi ya maofisa wa Serikali wakiwamo wa Uhamiaji wamefika maeneo hayo ili kubaini haya ambayo Watanzania hao wamesema ikiwamo kunyang'anywa pasipoti na mali zao, ili tujue kama ni kweli ili tukae na Serikali ya Msumbiji kujua nini cha kufanya," alisema.

Alisema Watanzania wapatao 3,000 wanaishi na kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii mjini Monte Puez na tangu operesheni hiyo ianze, raia 132 wamerudishwa nchini.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania waishio ughaibuni, kufuata sheria na taratibu za nchi wanamoishi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo