Chenji yampeleka darasa la kwanza mzee wa miaka 78


Frankius Cleophace, Tarime

Mzee Nyamhanga Suguta darasani
BAADA ya kusumbuliwa na hesabu ya chenji ya mauzo ya ndizi kwa wateja wake, Mzee Nyamhanga Gesaba (78) mkazi wa kitongoji cha Kibeyo kijijini Getenga wilayani hapa amejiunga na darasa la kwanza kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi juzi, mzee huyo alisema hakubahatika kwenda shule kwa sababu wazazi wake hawakumpeleka ingawa alipenda elimu.

Alisema alianza shule ya awali mwaka jana kabla ya shule anayosoma sasa kufunguliwa rasmi na Serikali.

Akifafanua sababu ya kuanza shule, Gesaba alisema amekuwa akipata shida kurudishia wateja wake chenji katika biashara yake ya ndizi anayofanya hivyo ili kuondokana adha hiyo ndipo akachukua uamuzi huo.

“Nikienda Tarime Mjini nashindwa kuongea Kiswahili, hivyo nimeamua kusoma hapa, ili nielewe Zaidi, nawaheshimu walimu wangu pia nawapenda wanafunzi wenzangu, lazima nitimize ndoto zangu licha na kuchelewa kusoma,” alisema.

Riziki Focus ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msngi Makerero anakosoma mzee huyo, alisema licha ya  mwanafunzi huyo kusoma, hatakuwa kwenye mfumo rasmi wa Serikali.

Hata hivyo, alisema wanasubiri Serikali ianzishe mfumo rasmi wa masomo ya watu wazima kwenye shule hiyo ili wamsajili rasmi.

“Mwaka jana alishakuwa mwanafunzi kabla ya kufunguliwa rasmi shule hii, lakini hakuwa kwenye mfumo rasmi endapo Serikali itaanzisha Idara ya Elimu ya Watu Wazima tutamsajili aendelee na masomo, lakini kwa sasa anafanya vizuri kwa sababu ameanza kuelea kuandika herufi,” alisema Mwalimu Mkuu.

Mwalimu wa Darasa analosoma mzee huyo, Magreth Albinus alisema alianza shule ya awali mwaka jana na amekuwa akifanya kazi zote shuleni hapo ikiwa ni pamoja na adhabu zinazotolewa bila kujali umri wake.  

Ofisa Elimu ya Msingi wa Halmashauri ya Wilaya, Emmanuel Johnson alisema mbali na mfumo rasmi, upo usio rasmi ambao unaruhusu mwananchi yeyote ambaye hakubahatika kupata elimu basi aipate nje ya mfumo huo.

Akasema pia kuwa kwa umri wa mzee huyo anaruhusiwa kujifunza mpaka ajue kusoma na kuandika na baadaye aendelee na shughuli zake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo