‘Ni ngumu kuenzi Ujamaa kama viongozi hawataki kukosolewa’


Suleiman Msuya 

Mwalimu Julius Nyerere
KATIBU Mwenezi wa zamani wa TANU na Mbunge mstaafu, Faustine Masha amesema ni vigumu katika nchi ambazo zimeruhusu mifumo ya kidemokrasia kufanikisha Mfumo wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa kile alichodai kuwa hakuna uvumilivu wa kisiasa.

Aidha, Masha ametoa siri ya siku nyingi kuwa iwapo watu wawili Mzee Daud Masasi na Balozi Paul Rupia wasingekubali Azimio la Arusha lisingekuwepo kutokana na nguvu ya kiuchumi ambayo walikuwa nayo wakati huo.

Masha aliyasema hayo jana wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la Arusha iliyoandaliwa na Kavazi la Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa uelewa wake, Ujamaa na Kujitegemea ungeweza kufanikiwa iwapo nchi ingeendelea katika mfumo wa chama kimoja, lakini kwa kuruhusu vyama vingi, falsafa hiyo itachukua muda kueleweka.

Mbunge huyo wa zamani alisema katika nchi ya kidemokrasia jamii inaishi kwa kukosoana hali ambayo haina nafasi katika nchi za kijamaa.

Alisema viongozi wakikosa uvumilivu wa kupokea kauli za kushutumiwa na kukosolewa ni wazi kuwa hakutakuwa na misingi ya ujamaa.

"Mimi ninavyoamini Azimio la Arusha lilijikita katika misingi ya ujamaa na kujitegemea na wakati ule utekelezaji ulionekana lakini katika mfumo wa leo ni vigumu kuona hilo likifanyika kwa sababu viongozi hawapo tayari umiliana," alisema.

Alisema mwalimu Nyerere aliamini katika Ujamaa na Kujitegemea, akiamini kuwa ndio njia sahihi ya kuchochea uzalishaji wa nchi na watu wake na si kutegemea watu wa nje.

Masha alisema ni wazi kuwa kauli mbiu ya mhadhara huo kuwa 'ujamaa wa Mwalimu umezimuliwa au umeteketezwa' kwa upande mmoja imeakisi uhalisia uliopo.

Katibu huyo muenezi ambaye pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha UDP alisema Azimio la Arusha haliwezi kurejea kwa kuwepo ni nia ya viongozi pekee bila wananchi kuwa tayari.

Kuhusu uwezekano wa Azimio kutopita iwapo Mzee Masasi na Rupia wasingekubali alisema hao ndio baadhi ya Watanzania wachache ambao walikuwa na nguvu ya kifedha wakati nchi imepata Uhuru.

Alisema iwapo matajiri hao wangepinga ni wazi kuwa Azimio lisingepita na misingi ya ujamaa na kujitegemea isingeonekana pia.

"Nakumbuka siku ile kulikuwa na ajenda 11 lakini ajenda ya Azimio la Arusha ilichukua kikao kizima lakini iwapo Masasi na Rupia wasingekubali hakuna kingeendelea ila baada ya Mzee Masasi kuunga mkono maamuzi hata Rupia hakuzungumza tukajua hoja imepita," alisema.

Alisema baada ya makubaliano hayo kupita Februari 5 mwaka 1967 utekelezaji ulianza ikiwa ni kutaifisha taasisi mbalimbali kama benki.

Masha alisema utekelezaji ulifanyika haraka kupitia Mwalimu Nyerere na yeye akiwa muenezi wa chama alifanikisha hilo kwa kufanya mikutano mbalimbali na kugawa vipeperushi.

Kwa upande wake mtoa mada Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Makerere, Ahmed Mohiddin alisema pamoja na changamoto zilizopo nchini Tanzania bado chembechembe za Azimio la Arusha na misingi yake zipo nchini akitolea mfano umoja, ushirikiano na utawala bora.

Alisema Nyerere aliamini katika misingi ya umoja na ushirikiano kwa Bara lote la Afrika hali ambayo ilichangia Tanzania kuheshimika duniani.

Prof alisema katika nchi kama Kenya mfumo wa uongozi unatenga wananchi na viongozi hali ambayo ni tofauti naTanzania.

"Mwalimu alitamani Afrika iishi katika misingi ya utawala wa Afrika na si kuiga tawala za nje ila hakueleweka hali ambayo inatutafuna hadi sasa," alisema.

Alisema katika kumfuatilia Mwalimu aligundua kuwa ni kiongozi asiye mbinafsi hali ambayo inagharimu viongozi wengi wa sasa.

Akichangia katika mhadhara huo Mkuu wa wilaya mstaafu Charles Sotola alisema kutofanikiwa kwa Azimio la Arusha kukichangiwa na viongozi kutolielewa.

Alisema viongozi waliowengi kunzia ngazi za juu hawana uelewa hali ambayo inachangia waje na mipango yao ambayo haitekelezeki.

"Baada ya kustaafu kupitia chama cha wakuu wa wilaya wastaafu nilikuja kugundua kuwa sisi ndio kikwazo katika mambo mengi ya maendeleo ikiwemo Azimio la Arusha," alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alisema Azimio la Arusha lilikuwa na misingi ya kusaidia mshikamano wa watu hivyo ni vema kukawa na mjadala wa pamoja ili kuirehesha nchi katika misingi hiyo.

Kwa upande wake Richard Mabala alisema Azimio la Arusha lilitekelezwa na vijana wazalendo kama Nyerere hivyo kutoa wito kwa Serikali kuwatumia ikiwemo kuwasikiliza wanachotaka.

Akizungumzia Azimio hilo Dickson Kamala alisema ni wakati wa kutenganishwa sasa na biashara ili kuhakikisha kuwa heshima na utawala bora unakuwepo kama Mwalimu alivyotaka.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo