Mbunge Chadema aipongeza Serikali


Mwandishi Wetu, Simanjiro

James ole Millya
MBUNGE wa Simanjiro, James ole Millya (Chadema) amepongeza viongozi wa Serikali kwa jinsi wanavyojali na kuhudumia wananchi.

Alitoa pongezi hizo juzi kwenye mikutano miwili ya hadhara Orkesumet na Mirerani wilayani hapa, baada ya kupewa nafasi kusalimia wananchi kabla Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hajazungumza nao.

“Serikali hii ina viongozi wachapakazi akiwemo Waziri Mkuu. Kwa mara ya kwanza katika jimbo hili, wananchi watapata maji safi kupitia mradi wa maji kutoka Mto Ruvu unaoendelea kujengwa sasa,” alisema akiwa Orkesumet.

Alitumia fursa hiyo kumwomba Waziri Mkuu afuatilie ujenzi wa hospitali ya wilaya, kwani sasa wanategemea kituo cha afya na hali ikibadilika inabidi mgonjwa apelekwe Arusha Mjini  umbali wa kilometa 150 kutoka hapo yalipo makao makuu ya wilaya.

Pia aliomba ijengwe barabara ya lami kuunganisha wilaya hiyo wilaya za Hai na Kiteto.

Akiwa Mererani, Ole Millya aliipongeza Serikali kwa kujenga barabara ya lami kutoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) hadi Mererani. Hata hivyo, aliiomba Serikali iongeze juhudi ili barabara hiyo iweze kufika Mirerani na Orkesumet.

Akijibu maombi hayo, Waziri Mkuu Majaliwa alimpongeza Mbunge huyo kwa uungwana wake wa kutambua juhudi za Serikali kwa wananchi wa jimbo lake.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara, aliwaambia wakazi hao kwamba Serikali itaendelea kufanya nao kazi bila kubagua kwa itikadi za kisiasa.

“Mmempa dhamana ya kuwawakilisha kama Mbunge wenu, lakini dhamana ya kuongoza nchi mmempa Rais John Magufuli kwa kuwapigia kura. Kwa hiyo, kazi yetu ni kuwatumikia ili tutatue kero zinazowakabili wana Simanjiro,” alisema.

Akizungumzia sekta ya afya, Waziri Mkuu alisema kituo cha afya cha Orkesumet kimepewa Sh milioni 49 kati ya Sh milioni 57 zilizoombwa ili kukiimarisha katika utoaji huduma za tiba.

“Tumeshatuma fedha zingine Sh milioni 163 kati ya Sh milioni 190 zilizoombwa ili kununulia dawa, vifaatiba na vitendanishi. Pia kuna Sh milioni 483 zimetengwa kuimarisha huduma za afya vijijini,” alisema.

“Nia yetu ni kujenga hospitali kubwa ya wilaya, lakini ni lazima tuimarishe miundombinu ya utoaji tiba ili wananchi wapate huduma stahiki. Ombi la hospitali ya wilaya nimelipokea na nitafuatilia kujua limefikia hatua gani,” aliahidi.

Kuhusu ujenzi wa barabara za kuunganisha wilaya, Waziri Mkuu alisema Serikali itaanza upembuzi na usanifu wa kina wa ujenzi wa barabara ya Arusha – Kiteto – Kongwa, ili ijengwe kwa kiwango cha lami.


Kuhusu migogoro ya ardhi iliyotajwa na wananchi kwenye mabango yao, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula aende na Mbunge huyo kwenye maeneo yanayolalamikiwa na wananchi ili kubaini kiini cha migogoro na aipatie ufumbuzi.

Kuhusu umeme, Waziri Mkuu alisema vijiji 18 kati ya 57 vya wilaya vimepewa umeme na vilivyokuwa vimeshaingizwa kwenye mpango wa Serikali wa kuvipatia umeme vijiji 8,000.

Alionya wakazi wa Mirerani akiwataka wachukue hadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI, kwani takwimu zinaonesha kuwa kasi ya maambukizi katika mji huo ni asilimia 18 kiwango alichosema ni kikubwa kuliko cha kitaifa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo