Samia ahimiza Ziwa Victoria litunzwe


Aidan Mhando, Mwanza

Mama Samia Suluhu
MAKAMU wa Rais, Samia Hassan Suluhu ametaka wataalamu wa Sayansi na watafiti Afrika Mashariki, kutumia Kongamano la Utafiti wa Kisayansi la Bonde la Ziwa Victoria kujadili na kutoka na majibu yatakayosaidia kutunza rasilimali za Ziwa hilo.

Akizungumza mjini hapa jana, akifungua  Kongamano hilo la siku mbili lililojumuisha viongozi wa nchi za Afrika Mashariki, wadau wa Sayansi, watafiti  na wakazi wa Mwanza, Makamu wa Rais alisema Ziwa Victoria linakabiliwa na changamoto nyingi, lakini zinaweza kupatiwa ufumbuzi kupitia kongamano hilo.

“Mkutano huu ni muhimu kwa nchi zetu za Afrika Mashariki ambamo Ziwa Victoria limo. Kuna changamoto nyingi ambazo zinalikabili, hivyo kupitia kongamano hili tunaweza kujadili njia sahihi za kutafuta ufumbuzi,” alisema Samia.

Alisema Ziwa Victoria ni chanzo kikuu cha uchumi kwa nchi za Afrika Mashariki, hivyo inahitajika mikakati sahihi ya kulisimamia ikiwamo utunzaji samaki wanaopatikana na rasilimali nyingine zilizopo ndani ya Ziwa hilo.

“Ziwa Victoria ni la kihistoria. Lina msaada mkubwa wa kiuchumi katika nchi zetu, linasaidia upatikanaji huduma za maji, hivyo uwepo wake ni muhimu tuendelee kulitunza vizuri kitaalamu ili liendelee kunufaisha nchi zetu,” alisema.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Greyson Lwenge alisema wanasayansi na watafiti wanaweza kuanzisha maendeleo endelevu ya kufanyia utafiti katika Ziwa hilo, ili kusaidia utunzaji wa rasilimali zilizopo.

“Changamoto kubwa kwa Ziwa Victoria ni uchafuzi wa mazingira unaotokana na magugumaji. Mabadiliko ya tabianchi pia ni changamoto ya utunzaji mazingira, hivyo watafiti na wanasayansi watasaidia utunzaji wa Ziwa na raslimali zilizopo,” alisema Lwenge.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Augustino Maiga alisema Ziwa Victoria ni kitambulisho thabiti cha nchi za Afrika Mashariki na lina historia ndefu, hivyo ni muhimu likatunzwa vizuri.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Ally Matano alisema lengo la kongamano hilo, ni kukutanisha wanasayansi kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazolikabili Ziwa hilo ambalo ni chanzo kikuu cha uchumi.              
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo