Mwigulu ajitosa dawa za kulevya


*Ataja mambo 5 atakayopambana nayo

Suleiman Msuya

Mwigulu Nchemba
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ametaja mambo matano makubwa, ikiwemo dawa za kulevya akisema wizara yake haina mjadala na suala hilo kwani linagusa maisha ya Watanzania wote.

Nchemba alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam baada ya kushuhudia viongozi mbalimbali wakiapishwa na Rais John Magufuli.

Walioapishwa ni pamoja na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga.

Wengine ni Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Omar Yusuph Mzee, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Joseph Sokoine na Balozi wa Tanzania nchini Uganda, Grace Mgovano.

Waziri Mwigulu alitaja mambo mengine ni kupambana na ugaidi, ujangili wa rasimali za nchi, uhalifu wa kutumia silaha na ubakaji.

Alisema wamejipanga kukabiliana mambo hayo kutokana na ukweli kuwa yamekuwa yakiongezeka kila kukicha hali ambayo inahatarisha amani ya nchi.

Mwigulu alisema wizara yake kwa sasa imekamilika kila idara hivyo ni wakati mwafaka wa kuhakikisha mapambano yote yanayohusika na mambo hayo matano yanafanikiwa.

Alisema dawa za kulevya ni janga linalohitaji ushirikiano wa kada zote hivyo wao wapo tayari kuhakikisha vita hiyo inakabiliwa kwa njia yoyote.

Waziri huyo alisema kwa siku za karibuni kumekuwepo na matukio ya ubakaji na ujangili hasa nyara za Serikali akisema waanamini kwa pamoja wataweza kupambana na wahusika.

“Tumejipanga kwa mambo makubwa matano ambayo ni dawa za kulevya, ujangili, ubakaji, uhalifu wa kutumia silaha na ugaidi ambapo vyote kwa pamoja vinashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu,” alisema.

Alitoa mwito kwa Watanzania kutoa ushirikiano wa mapambano mbalimbali ambayo yanafanywa na Serikali ili kudumisha amani ya nchi.

Tangu Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani imekuwa katika mkakati wa kupambana na matukio mbalimbali ya uhalifu ambapo kwa siku za karibuni mapambano hayo yameonekana kushika kasi hususan kwenye dawa za kulevya ambayo yalianzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo