Wanne walazwa kwa kipindupindu Kigamboni


Salha Mohamed

Hashim Mgandilwa
MKUU wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa, amesema wilaya hiyo ina wagonjwa wanne wa kipindupindu waliolazwa na 11 walitibiwa na kuruhusiwa kutoka hospitali.

Taarifa za ugonjwa huo zilitolewa Februari 18 mwaka huu baada ya mtu mmoja kufariki akiwa njiani kwenda hospitali baada ya kulalamika maumivu ya tumbo.

Mgandilwa alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo alifafanua chanzo cha ugonjwa huo wilayani humo.

Kwa mujibu wa Mgandilwa, ugonjwa huo umetoka katika familia mbili zenye watu 15, ambapo hadi sasa wagonjwa 11 wameruhusiwa kutoka hospitali huku wanne wakiwa bado wapo katika hospitali ya Vijibweni jijini humo.

“Kulikuwa na mtu mmoja alitoka Rufiji msibani, alipofika akawa analalamika tumbo ndipo wakaamua kumpeleka hospitali lakini kabla ya kufika, akafariki njiani,”alisema.

Alisema ndugu hao baada ya kuona ndugu yao amefariki, walimpeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti ili wafanye taratibu za mazishi.

Alisema familia hiyo haikufahamu kama ndugu yao amefariki kwa kipindupindu, bali waligundua baada ya kuumwa familia nzima.

“Baada ya kuona hivyo, Manispaa tumefanya juhudi za kuhakikisha ugonjwa huo hausambai ambapo tumefanikiwa kwani tusingefanikiwa, tungekuwa na wagonjwa zaidi ya 50,”alisema.

Mgandilwa aliwataka wananchi kuweka mazingira yao safi na kuchemsha maji ya kunywa, ili kuua vijidudu vinavyosababisha maradhi.

“Wananchi watunze mazingira yao yawe safi, wachemshe maji na si kunywa hivyo hivyo, lakini pia wapashe vyakula kabla ya kula,”alisema Mgandilwa.

Mgandilwa alitaja maeneo yaliyoathirika kuwa ni Kichangani na kubainisha kuwa hadi sasa wameshapiga dawa ili kuua vimelea vya ugonjwa huo na kuondoa madhara.

“Hakuna shule iliyofungwa, watoto wangu wanakwenda kama kawaida, tumepiga dawa na tunaendelea kutoa matangazo na elimu,”alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo