Manji atimiza ahadi yake Polisi


Celina Mathew
Yusuf Manji

MSHAURI Mkuu wa Kampuni za Quality Group, Yusuph Manji, jana aliripoti kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kama alivyoahidi juzi kutekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Manji alikwenda kituoni hapo kutokana na ahadi aliyoitoa juzi kwenye mkutano na wanahabari jijini humo, muda mfupi baada ya Makonda kumtaja akimtuhumu kuhusika na mihadarati kwenye mkutano wake na vyombo vya habari.

Manji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, aliwasili kituoni hapo saa 10:55 asubuhi akifuatana na wasaidizi wake wawili na wanasheria kadhaa.

Hata hivyo, gari lake lilizuiwa kuingia ndani ya eneo hilo, hivyo kulazimika kushuka na kutembea kuelekea ndani ya kituo hicho.

Wakati Manji akiingia, polisi waliimarisha ulinzi wa askari na gari la washawasha lililoegeshwa barabarani, huku baadhi ya watu wanaoaminika kuwa mashabiki wa Yanga wakitanda karibu kila kona ya eneo hilo.

Saa 5:29 Manji alitoka ndani ya kituo hicho na kusubiri hadi saa 6 mchana alipoingia tena ndani kwa mahojiano akiwa na wanasheria wake.

Saa 6:09 alitoka akiwa na wanasheria wake, lakini alipofika langoni kuelekea kwenye gari, askari mmoja alitoka ndani haraka na kumwomba arudi ndani.

Manji alitii na kurudi ndani ambako alihojiwa huku taarifa zikionesha kuwa wakati hayo yakiendelea si Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro wala Makonda aliyekuwapo.

Nje

Wakati Manji akiendelea kuhojiwa, baadhi ya wananchi walikuwa nje wakimsubiri lakini polisi waliwatawanya ili eneo hilo libaki wazi kutokana na wingi wao.

Wananchi

Baadhi ya wananchi walilaani hatua ya Makonda kutuhumu watu kwa kuwataja majina na kuwaita kupitia vyombo vya habari, badala ya mfumo rasmi kupitia mwito wa Polisi.

Wengine walimpongeza Manji kwa kwenda kuripoti kabla ya siku husika (leo) wakieleza kuwa alionesha utiifu bila shuruti.

Mkazi wa Keko, Temeke, Francis John alisema kitendo alichofanya Manji kwenda Polisi jana bila kusubiri siku ya mwito, kinapaswa kuigwa na viongozi wengine kwenda kusikiliza walichoitiwa.

"Kwa kweli Manji amefanya kitendo cha kiungwana nampongeza kwa kuwa shupavu, namsihi aendelee na moyo huo huo," alisema.

Salma Hamdani wa Magomeni, Kinondoni, alisema hatua hiyo ya Manji kuonesha kujali kwa kujitokeza Polisi inafundisha unyenyekevu na utii, lakini akasema viongozi wa Serikali wanapaswa kufuata taratibu, sheria na kuzingatia haki za binadamu katika kuteleza majukumu yao.

Ilipofika saa 10.27 jioni Manji na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Ujima, Josephat Gwajima waliondolewa kituoni hapo kwa gari Toyota Land Cruiser nyeupe namba T213ARS na kupelekwa kusikojulikana.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo