Tusiyasahau malengo na dira ya maendeleo


Mashaka Mgeta

ACHA NIPAYUKE

Mashaka Mgeta
MWAKA 1994, Serikali iliyoongozwa na Rais wa awamu ya tatu (mstaafu), Benjamin Mkapa, ilianza maandalizi ya kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa utekelezaji wa utakaofikia kikomo chake mwaka 2025.

Miaka mitano baadaye, yaani 1999, dira hiyo ilizinduliwa. Dira hiyo inajikita katika kusudio la kwamba ifikapo 2025, Tanzania iwe imepiga hatua zisizokuwa za kawaida katika mageuzi ya uchumi na maendeleo, ili kufikia hadhi ya kuwa taifa lenye kipato cha kati.

Miongoni mwa sifa stahiki kwa nchi itakapofikia hatua hiyo ni pamoja na ukuaji wa viwanda, kuhimili ushindani wa kiuchumi, maisha bora kwa wananchi, utawala wa sheria na kuwa na jamii iliyoelimika.

Unapoisoma Dira hiyo ambayo utekelezaji wake unahusisha mpango wa maendeleo wa miaka mitano, unaweza kubaini maeneo machache yaliyoainishwa, lakini yanayohitaji nyenzo, ushirikishi, rasilimali na uwezo wa kutambua, kutathimini na kupanga namna tofauti za utekelezaji wake, ili kufikia kusudio mahususi.

Unapoyapitia ‘maeneo’ kama ukuaji wa viwanda, kuhimili ushindani wa kiuchumi, maisha bora, utawala wa sheria na kuwa na jamii iliyoelimika ni rahisi kuyahesabu.

Lakini mipango, utekelezaji na kupima matokeo ni namna nyingine inayohitaji ushiriki mpana wa Taifa na washirika wake.

Ninatambua kwamba mipango kama ule wa miaka mitano na mikakati mbalimbali imewekwa ili kukidhi mahitaji ya Dira ya Maendeleo ya Taifa. Hoja ni je, hivi sasa Taifa lipo kwenye njia sahihi ya kufikia kusudio mahususi la dira hiyo?

Kupata jawabu sahihi la hoja hiyo kunahitaji kujielekeza katika utekelezaji wa kila sekta kwa mujibu wa majukumu na wajibu wake,iwe ni kwa upande wa umma na sekta binafsi.

Kupata jawabu sahihi kunahitaji kupima ushiriki wa Serikali katika kutimiza wajibu wake wa kuweka mazingira rafiki na yanayovutia uwekezaji, ushiriki wa umma na uboreshaji wa elimu utakaolifanya taifa kuwa na watu wenye uelewa mpana wa kupanga, kuchambua na kutathimini masuala tofauti ya kijamii.

Pia yapo mambo mengine kama uhuru wa habari na kujieleza, mgawanyo wa utendaji kazi kwa mihimili ya Taifa, ukuaji wa sekta binafsi inayoongoza kwa utoaji wa ajira na tegemeo katika uanzishaji wa viwanda.

Lakini yote hayo na mengine ambayo hayatajwa katika hoja hii, yanapaswa kuwa kwenye fikra za Watanzania, wakiitumia mipango na mikakati mingine kama nyenzo ya kufikia utekelezaji wenye tija wa dira hiyo.

Kwa hali ilivyo sasa, ingawa kwa kuzingatia ushahidi wa ki-mazingira, sehemu kubwa ya jamii katika sekta tofauti ni kama imeiweka kando Dira hiyo na sehemu za utekelezaji wake.

Mijadala inayohusu maendeleo na ustawi wa nchi na watu wake ni kama inaelekea ‘kufa’. Viongozi wachache wa umma hususan Rais John Magufuli, wanajikita katika kulirejesha taifa katika hoja zinazohusu ‘maeneo’ hayo.

Ingawa ni hivyo, Rais Magufuli pekee hawezi kufanikisha nia ama kusudio kuu lenye kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa, bali ushiriki mpana wa wasaizidi wake, wanataaluma, asasi za kijamii, vyama vya siasa, taasisi za kidini, vyombo vya habari na kada nyingine.

Kwa mfano, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilipotangaza matokeo ya kidato cha nne kwa waliohitimu mwaka jana, kuliibuka changamoto nyingi zinazoigusa sekta ya elimu, ikiwamo kuzidi kufanya vibaya kwa shule za sekondari za Serikali.

Changamoto nyingine ni ugumu wa wanafunzi kufaulu somo la hisabati katika kiwango kilichofikia asilimia 18.12, kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa kiswahili katika asilimia 77.75.

Ni nani hivi sasa anajadili kuhusu matokeo mabaya ya kidato cha nne kwa wanafunzi waliokuwa wanasoma shule zinazomilikiwa na Serikali?

Uhalisia na hoja za wanafalsafa wakiwamo Frederick Hegel, Aristotle, Plato na wengine, wamezungumzia umuhimu wa elimu katika kuifanya jamii ‘kutoka katika giza’ na `kuingia kwenye mwanga’, yaani kutoka kwenye ujinga kwenda kwenye welevu.

Unapofuatilia mijadala na matukio kwenye jamii, ni kama mambo muhimu kwa ustawi wa nchi ‘yanafunikwa’ kwa mbinu za kuibua jambo, hoja ama tukio, likafuatiwa na jingine, na jingine, jingine. Lililopaswa kuwa ajenda na mjadala kwa jamii linasahaulika, maisha yanaendelea.

Zipo changamoto nyingine zinazochangia nyingi zinazochangia kudumaa kwa huduma za kijamii kama afya, kilimo, viwanda, biashara, ufugaji, maji nakadhalika.

Vipo vitendo vinavyohatarisha haki, usawa na usalama wa watu na mali zao; kwa mfano kuibuka kwa vikundi maarufu kama ‘panya road’. Kuwapo kwa mazingira magumu ya kufanya shughuli za kiuchumi hivyo kuchangia biashara kadhaa kufungwa na waajiriwa wakarejea mtaani. Nani anayejadili hayo?

Taifa halina wataalamu wa uchumi, biashara, hifadhi ya jamii, maendeleo na ustawi wa watu? Hakuna sekta binafsi? Changamoto hizo zinazosikika kila kona nchi haziwafikii walengwa ili waishauri Serikali na kwa ushirikiano wa pamoja ipatikane suluhu yenye tija kwa nchi na watu wake?

Wakati hayo yakitokea, Tanzania imeendelea kuwa nchi mwanachama wa jumuiya za kikanda na kimataifa zinazoshirikiana katika nyanja tofauti zikiwamo zile zinazozorota ndani ya nchi. Katika hali hiyo, Watanzania watawezaje kumudu ushindani dhidi ya raia wa mataifa mengine?

Kwa maoni +255754691540
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo