Wavuvi wagoma Kanda ya Ziwa


Charles James

WAVUVI wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa wamegoma kuvua samaki wakipinga nyanyaso kutoka kwa Serikali kuhusu utata wa kipimo cha urefu wa nyavu kinachopaswa kutumiwa.

Wavuvi hao wameamua kugoma baada ya mfululizo wa vitendo wanavyodai kuwa ni vya uonevu kutoka kwa maofisa wa uvuvi na askari wa doria jijini Mwanza wanaowakamata kwenye operesheni zao za usiku ziwani.

Hivi karibuni wavuvi 14 walikamatwa Bugogwa, Igombe, wilaya ya Ilemela na kunyang’anywa nyavu zao zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Sh milioni 50.

Akizungumzia suala hilo la mgomo, Mbunge wa Viti Maalumu Suzan Masele alisema athari za mgomo huo zimeanza kuonekana kuanzia kwa wananchi wa kawaida wanaotegemea samaki kwa kitoweo au biashara za mama ntilie, lakini pia kwa viwanda vya samaki vinavyozalisha kwa kutegemea samaki wanaovuliwa na wavuvi hao.

“Kinachoshangaza badala ya Serikali kujikita kujadili njia za kutatua mgogoro huo kwa kukutana na wavuvi na kuwaelimisha juu ya urefu wa nyavu unaotakiwa, wamesema wanaunga mkono mgomo huo kuendelea ili kusaidia samaki kuzaliana,” alisema Suzan.

Alisema kauli hiyo imethibitisha kuwa Serikali ya Mwanza imeshindwa kuangalia athari wanazopata wananchi kutokana na mgomo huo na endapo utaendelea bila ufumbuzi wa haraka utadhihirisha kuwa Serikali ya Mkoa imeshindwa kutekeleza majukumu yake.

“Tumewasikia wavuvi kupitia vyombo vya habari wakisema wako pamoja na Serikali kupinga uvuvi haramu hasa wa makokoro na milipuko na wako tayari kusaidiana kuwapata na kuwadhibiti wanaofanya vitendo hivyo, sasa kwa nini wasikae nao na kuwasikiliza?” Alihoji Mbunge huyo.

Alitoa mwito kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuingilia kati na kumaliza mgogoro unaoendelea baina ya wavuvi hao na Serikali ya Mkoa ili kusitisha mgomo wao kabla athari hazijawa kubwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo