Mpinga azuia magari ya IT kubeba abiria


Leonce Zimbandu

Mohamed Mpinga
KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga, amewapiga mafuruku abiria kupakiwa kwenye magari yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi yenye namba inayoanza na IT, licha ya kipato duni cha madereva wake.

Mpinga alisema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Madereva na Wadau wa Magari Yaendayo Nchi Jirani (ITDA), uliohudhuriwa na mamia ya wanachama hao.

Mpinga alisema lengo ni kupunguza ajali za magari ya IT ambayo hayajasajiliwa rasmi kutoa huduma za usafiri, hivyo kitendo cha kutoa huduma ni kinyume na sheria za nchi.

Alisema ni wajibu wa kila dereva kuzingatia sheria za usalama barabara kwa mujibu wa maadili ya udereva, ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

“Unajua ilitokea ajali moja mkoani Morogoro baada ya gari la IT kugongana na gari lingine, abiria aliyekuwa kwenye gari la IT alikufa lakini dereva alipata majeraha tu,” alisema.

Mwenyekiti wa ITDA, Jimmy Mwalugelo alisema wananchama wake wanakabiliwa na changamoto ya mawasiliano kati ya dereva na mwagizaji, hali inayowafanya kuishi maisha magumu.

Alisema madereva hao hawana ajira wala mkataba, lakini wanazo leseni za udereva zinawapa sifa ya kuendesha magari hayo, hivyo itakuwa vyema kwa Serikali kuwatambua rasmi.

“Tunasubiri mpango wa kutumia vibao vyenye rangi nyekundu, bendera na stika ambayo itakuwa na jina la dereva, ili kuepuka udanganyifu na kuongeza umakini kwa dereva,” alisema.

Mwakilishi kutoa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Johansen Gaitano, alisema suala hilo la kutambua chama hicho, linapaswa kushirikisha wadau mbali mbali, wakiwamo waagizaji wakubwa wa magari.

“Iwapo wadau wote watakubali na kutambua chama cha ITDA itakuwa rahisi katika utekelezaji wake kuliko ilivyo sasa lakini Serikali tayari imewapokea,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo