Polisi yakanusha kushikilia wageni


Mwandishi Wetu

Kamanda Charles Mkumbo
JESHI la Polisi mkoani hapa limekanusha kuwashikilia raia tisa wa kigeni waliodaiwa kughushi nyaraka za kuishi na kufanya kazi nchini.

Badala yake Jeshi hilo kupitia Kamanda wake wa Mkoa, Charles Mkumbo, limekiri kuhoji raia watatu wa kigeni ili kusaidia ushahidi wa taarifa zilizolifikia Jeshi hilo na Idara ya Kazi mkoani hapa kuhusu uhalali wa vibali vya raia hao kufanya kazi nchini.

Wageni hao ni wafanyakazi wa kampuni ya uwindaji wa kitalii ya TGT ya Ngaramtoni mkoani hapa, ambayo imekuwa ikifanya uwindaji huo tangu mwaka 1990.

Waliohojiwa na uraia wao kwenye mabano ni Cliff Duvell Hunter (Afrika Kusini), Nana GrosseWoodley (Ujerumani) na Nicolas Carel Stubbs (Afrika Kusini).

Kamanda Mkumbo alisema jana kwamba baada ya kuwahoji waliwaacha kwani walifuata taratibu zote za kupata vibali hivyo, ingawa baadaye viligunduliwa kuwa vya kughushi.

“Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa wageni hao walifuata utaratibu wote ikiwa ni pamoja na kulipa ada na tozo zinazotakiwa lakini wakapewa vibali vya kughushi, tuliwahoji na kuwaacha,” alisema Mkumbo na kuongeza:

“Inaonekana vibali hivyo vilighushiwa na maofisa wa Serikali huku wageni wakiwa hawajui lolote, hivyo kwa unyeti wa suala hilo, kikosikazi maalumu kinafuatilia ili kupata undani wake.”

Uchunguzi unaonesha kushikiliwa kwa maofisa wawili wa uhamiaji kutoka Manyara, Juma Fakhi na mwingine wa TGT ambaye hakutajwa jina kuhusu sakata hilo la vibali.

Kamanda Mkumbo alithibitisha kukamatwa kwa maofisa hao kutokana na vibali hivyo tisa vilivyolipiwa dola 5,000 za Marekani.

Mkumbo alisema jalada la maofisa hao liko kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusubiri maelekezo ya kisheria.

Mmoja wa wajumbe wa kikosikazi hicho, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema mchezo huo wa kughushi vibali umekithiri mkoani hapa, huku maofisa Uhamiaji na wa Idara ya Kazi wakinyooshewa vidole kuwa vinara wakuu.

“Tatizo hili limekithiri sana mkoani hapa kutokana na kuwa na wageni wengi wafanyao kazi hapa. Wageni wanadanganywa sana kwa kupewa vibali feki huku serikali ikikosa mamilini ya fedha za kigeni kila mwaka…zinaishia mikononi mwa wajanja wachache, uchunguzi wetu utabaini mengi,” alisema.

Aliishukuru TGT kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kikosikazi hicho, akiamini hatua hiyo itachimbua mzizi wa tatizo hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TGT, Michelle Allard alipotakiwa kuzungumzia kadhia hiyo kwa njia ya simu, alisema kwa sasa hawezi kusema lolote hadi uchunguzi wa kikosikazi hicho utakapokuwa umekamilika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo