Wasanii zaidi waongezwa kwenye tuhuma za ‘unga’


*Ni Vanessa Mdee, Tunda Sabasita, wakacha
*Makonda atoa agizo kukutana nao Jumatatu

Salha Mohamed

WASANII wawili Vanessa Mdee na Tunda Sabasita ‘Video Queen’ ni miongoni mwa watuhumiwa wapya walioongezwa kwenye orodha ya walioitwa Polisi kwa mahojiano, kutokana na kutajwatajwa kwa utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya.

Mbali na wasanii hao wawili, wanne kati ya watano wa mwanzo kuitwa, walifika jana kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa mahojiano, wakiongozwa na aliyekuwa Mnyange wa Tanzania 2006, Wema Sepetu, ambaye alionekana akilia kituoni hapo muda mwingi.

Wasanii wengine waliowasili kituoni hapo kwa mahojiano ni Khalid Mohamed ‘TID’, Hamidu Chambuso ‘Nyandu Tozi’ na mwingine aliyetajwa kwa jina la Babuu wa Kitaa.

Akizungumza jana Dar es Salaam baada ya kuwasili kwa wasanii hao Polisi, Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda alitaja orodha ya watuhumiwa watano iliyoongezeka, akiwemo Vanessa na Tunda. Wengine ni maaskari Mudy Zungu, Fadhil na Beni.

”Hawa watatu Kamishna waunganishe kwenye orodha ya wengine muanze kushughulika nao, kuna mwingine anahangaika kununua nyumba Kigamboni kupitia hizi fedha za dawa za kulevya, mimi nipo na nitaendelea kuwepo na tutafanikiwa,” alisema.

Makonda alimtaka Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro ifikapo Jumatatu awe amekamata watuhumiwa waliotakiwa kufika kituoni hapo jana lakini hawakufika.

“Vita hivi haviishi leo, vitakwisha dawa zitakapokwisha lakini vita hivi si vya Kamishna Sirro, si vya Rais Magufuli (John), wala Makonda bali ni kila mkazi wa Dar es Salaam, kwani tunaishi nao, tunakula nao, tunacheza nao na wengine ni wafadhili wetu.

“Nimegundua na limenishitua na litafanyiwa kazi, huwezi kuwa na askari aliyekwenda kukamata dawa za kulevya, halafu akachukua na kuuza, sasa alimwuzia nani?

“Halafu huyo huyo askari bado yumo kwenye utumishi, anahudumia wananchi kama askari ni sawa na majambazi tu,” alisema.

Alisema hawawezi kuendelea kuwa na baadhi ya watumishi wanaochafua Jeshi la Polisi na kuchafua heshima ya Kamanda Sirro.

“Askari wengine ndani ya hizi wiki mbili walichukua fedha za dawa za kulevya Sh bilioni moja na kugawana, na wanaishi kwa raha mjini wakati sisi na Rais Magufuli tunapambana na dawa ili ziishe, askari wanafanya hiyo kazi. Mimi mtandao huu lazima utokomee.

“Wananchi wanazidi kuhamasika na kuona kumbe Serikali ya Magufuli inatokomeza dawa, kwa imani zao wanaendelea kutoa taarifa, nina majina ya watu watano na wa sita yuko China anaingiza dawa mwezi huu, nimeagiza Uhamiaji akiingia tu wamtie nguvuni,” alisema Makonda.

Aliwataka wananchi watambue kuwa vyombo vya Dola viko imara na hawatasita kuwachukulia hatua wanaokwenda kinyume na maadili ya utumishi.

Alisema wananchi wana wajibu wa kuhakikisha wanashiriki mapambano hayo na kushinda.

Alisema jambo hilo si la wasanii peke yao bali wengine wa kawaida na kumtaja Omary Sanga kusababisha zaidi ya asilimia 65 hadi 75 ya Watanzania kufungwa China.

“Sasa hivi yuko Dubai anajiandaa kwenda China, lakini mkono wa Magufuli ni mrefu tutamkamata, wengine Kashozi, Amani, Halidali Kavila, Tunda hawa wote nawahitaji Jumatatu saa mbili asubuhi akiwamo dada yangu kipenzi Vanessa,” alisema.

Makonda alisema furaha yake ni kuona mkoa unapona ili hata mikoani kuwe salama na heshima ya mkoa iliyoasisiwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume inarudi.

Kamanda Sirro alisema tayari Jeshi lake limeunda timu maalumu ya kushughulika na wanaojihusisha na dawa za kulevya chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Mkoa huo, Makonda.

“Timu hii imeundwa na idara zote si polisi peke yao, lengo ni kutokomeza dawa za kulevya Dar es Salaam, tuko vizuri,” alisema.

Sirro alisema katika tano walikamata kete tatu huku akibainisha kuwa operesheni hiyo ni endelevu.

Alisema hadi sasa polisi 10 wamekamatwa huku wawili wakiwa nje ya mkoa na taratibu za sheria zinafuatwa ili wakamatwe.

Idadi hiyo inafanya jumla ya askari kuwa 15 wakidaiwa kujihusisha na uuzaji na utumiaji dawa za kulevya.

Wema alifika kituoni hapo mapema jambo lililofanya waandishi kutomwona wakadai amepita mlango wa nyuma.

Kutokana na hali hiyo, iliwalazimu polisi kumtoa nje na kupanda gari namba T 811 DJK na kuzunguka jengo hilo na kuingia tena na waandishi kumwona na kumpiga picha naye akashindwa kuhimili na kulia.

Wasanii wengine waliowasili kituoni hapo ni TID, Nyandu tozi na Babuu wa Kitaa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo