Joyce Anael, Same
WATUMISHI wa umma ofisini na wananchi
kwa ujumla wameshauriwa kuanza utaratibu wa kunywa kawaha ili kukuza uchumi wa
mkulima na pato la Taifa.
Mbali na kukuza uchumi, pia unywaji wa
kahawa unaburudisha mwili na kupunguza uwezekano wa magonjwa ya saratani ya
ngozi na ini.
Majid Kabyemela ambaye ni Ofisa Kilimo,
Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya ya Same, alisema hayo jana kwenye maadhimisho
ya Siku ya Unywaji Kahawa wilayani humo na kuongeza kuwa faida ya unywaji kahawa
ni pamoja na kuchangamsha mwili pia kusaidia kufikiria kwa haraka na kupunguza
kisukari.
Alisema wananchi wanaokunywa kahawa
wanapata faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuzuia ugonjwa wa kutetemeka, gauti,
magonjwa ya moyo kwa wazee na kupunguza mafuta mwilini kwa wenye uzito mkubwa,
hivyo kuna haja ya wananchi kujijengea utamaduni wa kunywa kahawa.
Kabyemela alisema kahawa ni moja ya
mazao ya biashara nchini na huliingizia Taifa kiasi cha fedha za
kigeni ambapo mwaka 2014/15 zao hilo,
liliingizia Taifa dola 135,768,630 za Marekani huku msimu wa mwaka 2015/16 hadi
Aprili Taifa lilipata dola 132,319,519.
Alisema kahawa humwingizia mkulima kiasi
cha Sh 2,310,300 kwa ekari moja kwa mwaka kwa mkulima anayetunza shamba vizuri
kwa kufuata kanuni nane za kilimo cha kahawa na amri 10 za usindikaji kahawa
ili kupata daraja la juu ambalo lina bei nzuri.
Ofisa huyo alitaja sababu zinazochangia
kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo, kuwa ni pamoja na bei ndogo ya zao hilo
inayowakatisha tamaa, baadhi ya wakulima wanaotaka kujiingiza kwenye kilimo cha
kahawa, upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima wenye uwezo mdogo na mabadiliko ya
tabianchi yanayosababisha uhaba wa mvua na hivyo kuathiri uzalishaji.
Alitaja sababu zingine za kushuka kwa
uzalishaji wa kahawa ni pamoja na wakulima kukimbilia mazao ya biashara ya
haraka yenye faida kubwa kama tangawizi
na kuacha kulima kahawa, uwezo mdogo wa wakulima kununua miche ya kahawa
na kubadili mibuni mikongwe na wadudu waharibifu.
Wilaya ya Same ina wakulima 1,722 huku
hekta zinazolimwa kahawa zikiwa ni 1,600 ambapo mwaka 2015/16 jumla ya tani 320
zililimwa na kuwaingizia kipato wakulima na pato la Taifa.
0 comments:
Post a Comment