Sikuwachagua mpige dili—Simbachawane


Seif Mangwangi, Arusha

George Simbachawene
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, amesema amewateua wajumbe wa bodi ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) ili kufanya kazi ya wananchi na sio kupiga dili kupitia mfuko huo.

Pia, amesema migogoro mingi ndani ya mashirikia ya Serikali imekuwa ikichangiwa na wajumbe wa bodi kutaka kufanya biashara na madalali na kusahau kazi zao kama waelekezi na wasimamizi wa menejimenti.

Simbachawene aliyasema hayo jana jijini hapa alipokuwa akizindua bodi ya wadhamini ya mfuko wa LAPF ambayo itafanyakazi yake kwa miaka mitano huku akisisitiza uadilifu kwa wajumbe.

Aliwataka wajumbe kuendeleza mambo mazuri yaliyofanywa na bodi iliyomaliza muda wake na kuwataka kuzalisha ajira katika sekta ya viwanda ili kukuza ajira sanjari na kusimamia maslahi ya wanachama kwa kuondoa malalamiko ikiwemo kulipa mafao yao kwa wakati.

"Ni vyema wajumbe wa bodi mkaepuka migogoro kwa kufanya biashara za dili na madalali wa pembeni badala yake msimamie rasilimali za mfuko huu kwa uadilifu na weledi kwa maslahi ya nchi na wanachama wenu," alisema.

Alisema ni vyema mfuko huo ukaangalia aina ya uwekezaji katika sekta ya viwanda utakaoibua ajira kwa vijana ikiwemo kuondoa malalamiko baina ya wanachama na menejimenti ya LAPF.

"Bodi hii niliyoichagua ni bodi yenye wasomi wengi na haina wanasiasa hapa, ukweli wa Mungu sijaagalia urafiki wakati wa uteuzi, fanyeni kazi kwa weledi na kuepukana na dili ambazo hazitaleta tija katika mfuko huu, menejimenti ni bodi mshirikiane katika kuhakikisha mfuko huu unajivunia ile kauli mbinu ya kulipa jana hivyo zingatieni ushauri mnaopewa na wataalam na fanyeni kazi hoja mbalimbali na kisha kutoa maelezo," alisisitiza.

Aidha Waziri Simbachawene aliitaka bodi hiyo kudhibiti gharama za uendeshaji wa mfuko na kujenga mahusiano mazuri kati ya menejimenti na bodi kwaajili ya kuleta ufanisi nzuri wenye tija na mafanikio.

Mwenyekiti mpya wa bodi hiyo, Profesa Faustine Bee ambaye ni Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha biashara cha Ushirika Moshi, Kilimanjaro alimshukuru Rais John Magufuli kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo yenye jumla ya wajumbe saba wa Kada mbalimbali.

Wajumbe hao wengine ni pamoja na Dk Rehema Kilonzo anayetokea chuo Kikuu cha Dodoma, Suleiman Kikingo, Henry Kabatwa, Wakili Cornelius Kariwa pamoja na Tumaini Nyamhokya

Mkurugenzi wa mfuko huo, Eliud Sanga alisema mfuko huo wa Lapf ni mfuko wa kipekee unaojali wanachama sambamba na kupokea tuzo mara sita mfululizo ya utunzaji wa hesabu huku ikiwa na mikakati ya kuinua sekta ya viwanda na kuzalisha ajira kwa watu mbalimbali.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo