Mgeja ataka Bunge liongeza makali kwa Serikali


Mwandishi Wetu

Khamis Mgeja
WABUNGE wameshauriwa kuzidi kunoa meno ya Bunge kama lilivyokuwa Bunge la Tisa na kuepuka kuwa tawi la Serikali kwa kuhakikisha inaisimamia Serikali, kuishauri na kuipa maelekezo kwa mujibu wa Katiba.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Tanzania Mzalendo Foundation, Khamis Mgeja.

Alisema kuwa anatambua mara kadhaa imetokea wabunge kusimamia maslahi ya vyama katika shughuli za kibunge, jambo ambalo limekuwa halina tija kwa taifa na kuwakumbusha wabunge kuwa wao ni wawakilishi wa wananchi waliowachagua na si vyama.

Ili kuhakikisha wanasimamia misingi yao ya kibunge, wanapaswa kuwa na kuli mbiu ya kutanguliza Tanzania kwanza na kuyaweka kando maslahi ya vyama vyao. Wanapaswa pia kuona umuhimu wa kujadili mambo makubwa yanayolitafuna taifa kwa uwazi kama ambavyo wamediriki kuzungumzia ukame na njaa inayoelekea kulikumba taifa.

“Hapa tulipofikia kwa mwenendo wa Serikali yetu Bunge halina budi kunoa meno. Lisimamie misingi yake ambayo ni kuwakilisha umma uliowachagua na si kuangalia matakwa ya vyama vyao ama kuwa wakala au tawi la serikali, bali lisimame kwa mujibu wa Katiba,”alisema Mgeja.

Alisisitiza kuwa Bunge halipaswi kuitetea Serikali katika kukandamiza demokrasia kwa kukomoa vyama vya upinzani kutofanya mikutano,pia kuvifunga midomo vyombo vya habari kwa kuvitungia sheria kandamizi hatua ambayo itachochea usiri na ubadhiru,na ukiukwaji wa utoaji haki kwa umma.

Aidha aliwaomba wabunge hao kutoa msimamo wa pamoja juu ya hatima ya Katiba mpya kwa sababu mchakato wake umetumia mabilioni ya fedha za Watanzania.

Mgeja ambaye mbali ya kuongoza taasisi hiyo, pia ni Kada maarufu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), aliwakumbusha wabunge hao kuhoji Serikali sababu iliyofanya baadhi ya nchi kusitisha misaada ya ufadhili kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar,kama vile MCC la nchini Marekani,ambapo ufadhili wa fedha hizo zilikuwa muhimu kwa ustawi wa Taifa.

Alikumbusha Bunge hilo litambue kwamba umaskini wa Watanzania na nchi kwa ujumla unasababishwa na kutosimamia vizuri  rasilimali za nchi,na kuwaomba kuhakikisha wanapitia upya kwa uwazi mikataba ya wawekezaji ambao kipindi hiki wanavuna rasilimali.

“Nawaomba wapitie upya na kwa uwazi mikataba ya Madini,Gesi,mafuta na makaa ya mawe,mashamba,viwanda zikiwemo na rasilimali zingine;ikiwemo Nishati ya Umeme;kuona kama ina manufaa ya Nchi,pindi Bunge likibaini haina liweke azimio la kuifuta,”alisema Mgeja.

Pia aliwaasihi katika kuhakikisha rasilimali za nchi zinanufaisha wananchi kabla ya mikataba mipya kufungwa,ni budi wakajifunza katika baadhi ya Nchi ambazo zinanufaika na rasilimali zao,zimetumia mbinu gani kufanikisha hilo.


Katika kuhakikisha Bunge linatekeleza na kusimamia majukumu yake ni vyema likahoji  kuhusiana na ununuzi wa ndege mbili zilizonunuliwa na serikali je sheria za manunuzi zilifuatwa pia mkataba kati ya serikali  na ATCL kuwa wazi kwakuwa hizo fedha ni za umma walipa kodi hivyo wangependa kujua kupitia bunge.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo