Wafuasi wa Lipumba wahofia usalama wao


Celina Mathew
MGOGORO wa CUF umeendelea kupata sura mpya, baada ya upande wa Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba, kutoa kauli ikionesha hofu ya usalama wao na ofisi za chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi hizo jana,   Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CUF, Masoud Mhina alidai kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, Julius Mtatiro na wenzake, wamepanga kuvamia ofisi za chama hicho.

Mhina alidai tayari walinzi wa chama wamejipanga kukabiliana na kikundi chochote chenye dhamira ya kuhujumu chama hicho.

“Tuna taarifa kuwa kuna vijana wanaandaliwa kuja kuvamia ofisi kuu za chama Buguruni kwa ajili ya kufanya vurugu, nadhani wanatufahamu vizuri, tukianza huwa hatukamatiki na tutahakikisha chama kinabaki salama,” alidai.

Mhina alidai wanawafahamu viongozi waliopanga hujuma hizo na tayari wamewasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu vitisho na vitendo vya udhalimu vinavyokusudiwa kufanywa na wasaliti wa chama hicho, dhidi ya viongozi wa chama upande wa Bara.

Alidai kwa sasa hawawezi kuweka wazi majina ya viongozi hao kwa kuwa wanajijua na vikao wanavyofanya kila kukicha ila ipo siku watawataja ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria na kikatiba.

“Tutawashughulikia kisheria na kikatiba wanaotaka kuhujumu chama kokote waliko tutawatafuta hadi maeneo ambayo wanafanyia mikutano na kuwakamata, maana CUF hatuna mgogoro, ulishamalizwa na Msajili wa Vyama vya Siasa,” alidai.

Mhina alitoa onyo kwa wanaojiita viongozi wa CUF wanaozungumzia vichochoroni na kuwataka kama ni halali, waache na badala yake waende ofisi za chama hicho ili wamweleze Profesa Lipumba walipewa uongozi na nani.

“Tumewavumilia sana kiasi cha kutosha, sasa dawa yao ipo jikoni mmoja mmoja baada ya mwingine tutawajibika nao, hivyo nachukua nafasi hii kutoa onyo kwao kama ni viongozi, bora waje ofisini si kuzungumzia vichochoroni,” alisema.

Awali akizungumzia kazi za Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Chama, Mhina alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF ibara ya 88 (2) (a), Katibu atakuwa Mtendaji Mkuu wa Kamati na Ibara ya 87 (1) imeeleza kuwa wajibu wa Kamati hiyo ni kuhakikisha usalama wa chama unakuwapo nchini.

Alitumia nafasi hiyo kumsihi Katibu Mkuu aache vikao vya kuhujumu chama, kwa kuwa havina tija kwake zaidi ya kujenga uhasama dhidi ya wanachama na viongozi hao Bara na Zanzibar.

Akizungumzia tuhuma hizo, Mtatiro alihoji kuwa tangu lini Mwenyekiti wa Chama akachaguliwa na Msajili na kuongeza kuwa Buguruni pamejaa wahuni wanaomlinda Lipumba, hivyo hawawezi kufika eneo hilo.

“Hatuwezi kufanya upuuzi kama huo wa kwenda pale na hakuna anayetaka kuvamia, kwa kuwa hakuna anayetaka kukaa kwenye ofisi ile kimabavu kama Lipumba, tena kwa msaada wa wahuni na Polisi, sasa tunakwenda kuhujumu nini na ili iweje?”Alihoji.

Alihoji wanaojiita wakurugenzi, wameteuliwa na nani wakati hawamtambui Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF.

Kwa mujibu wa Mtatiro, ili mtu awe Mkurugenzi lazima ateuliwe na Mwenyekiti halali wa chama anayetambuliwa na vikao vya kitaifa hivyo haelewi waliteuliwa na nani.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo