JPM awapa jeuri machinga wa Soko Matola


Venance Matinya, Mbeya

AGIZO la Rais John Magufuli kutaka machinga wasibughudhiwe, limezua sintofahamu kwa viongozi wa halmashauri ya Jiji la Mbeya, baada ya wafanyabiashara hao kutoka nje ya soko na kujenga mabanda kwenye maeneo yasiyostahili.

Sintofahamu hiyo ilitokea juzi, baada ya machinga hao wapatao 24 kuamua kujenga vibanda vya biashara nje ya Soko la Sokomatola kinyume na taratibu, huku wakisisitiza kuwa wanafuata Kauli ya Rais kwamba hata ikiwezekana wafunge hata barabara ili wafanye biashara zao.

Kutokana na hali hiyo, Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya ulibomoa vibanda hivyo, hali iliyozua vurugu baina ya mgambo wa Jiji na wafanyabiashara hao wakidai waachwe waendelee na biashara, licha ya kukiri eneo hilo haliruhusiwi kwa mujibu wa sheria.

Akizungumza katika kikao cha usuluhishi ambacho kiliitishwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David Mwashilindi na kuhudhuriwa na Mbunge wa Mbeya mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Zakaria Machoa alisema kwa mujibu wa sheria wafanyabiashara wakihitaji eneo la biashara lazima waandike barua ambayo itapita serikali ya Mtaa, Kata kisha Halmashauri.

Alisema wafanyabiashara hao walijiamulia wenyewe bila kufuata taratibu za kuomba kupanua eneo la soko ili waweze kuuzia nje ya Soko kwani hata Ofisi ya Serikali ya Mtaa haikuwa na taarifa wala Ofisi za Kata, pia hazikuwahi kupokea barua za maombi kutoka kwa wafanyabiashara hao.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Soko la Sokomatola, Abdalah Shaibu alikiri kuandika barua ya kuomba kupatiwa eneo, lakini haikujibiwa hadi hapo wafanuabiashara walipoamua kuanza kujenga vibanda ili wafanye biashara kutokana na ufinyu wa maeneo na kusisitiza kuwa uamuzi waliochukua ni kuunga mkono kauli ya Rais Dk. Magufuli.

Aidha baadhi ya Wafanyabiashara waliobomolewa vibanda vyao walikiri kufanya ujenzi huo kinyume cha taratibu ambapo waliuomba uongozi wa Jiji kutumia busara kuwaruhusu kuendelea kufanya biashara katika eneo hilo hadi utaratibu mwingine utakapotolewa.

“Nikuombe Mkurugenzi na Meya tumieni Busara kama ilivyotumika katika masoko mengine kama Kabwe na Mwanjelwa mturuhusu tufanye biashara kule ndani hakutoshi na sisi tupo tayari kulipa ushuru na kufuata taratibu zote” alisema Beth David Mfanyabiashara Sokomatola.

Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi (SUGU) alisema msimamo wake tangu 2010 ni kuona kila mwananchi anapewa haki ya kujitafutia riziki hivyo anaungana na wafanyabiashara kumuomba Meya awaruhusu kufanyabiashara eneo hilo kwa masharti ya kuzingatia usafi wa Jiji.

“Mimi kama Mbunge nabariki Wafanyabiashara kuendelea na biashara katika eneo hili lakini tuzingatie usafi na maboresho mengine ya kuhamisha au kutafuta eneo lingine tutafuata taratibu za vikao hivyo naomba Mheshimiwa Meya waruhusu watafute riziki wananchi hawa” alisisitiza Sugu.

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Mchungaji David Mwashilindi alisema Halmashauri ya Jiji limewaruhusu kufanya biashara eneo hilo kwa muda hadi watakapotafutiwa eneo la kudumu kwani kinachotakiwa ni Halmashauri kuwa na amani na utulivu.

Aliongeza kuwa wataendelea kuwepo hapo hadi pale utaraibu wa kuwaondoa wafanyabiashara wote wanaofanya maeneo ambayo hayaruhusiwi hususani barabarani kwa kuwatafutia maeneo ya kwenda kabla ya kuwaondoa kabisa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo