Bunge laingilia kati makontena 282 ya mchanga ya dhahabu


*Watendaji wapishana kauli kiwango cha dhahabu kinachosafirishwa nje ya nchi
*Acacia watangaza hasara Sh, bilioni 40

Fidelis Butahe

BUNGE limeingilia kati sakata la kuzuia makontena 282 yenye mchanga wenye dhahabu katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo Spika, Job Ndugai ametangaza kuundwa kwa timu ya wabunge kuchunguza jambo hilo, pamoja na kupitia mikataba yote ya madini.

Wakati hayo yakiendelea, Kampuni ya Acacia inayoendesha migodi ya Buzwagi na Bulyang’ulu imetangaza kupitia mkurugenzi wake, Brad Gordon kuwa tangu kuzuiwa kusafirishwa mchanga huo, wamepata hasara ya takriban Sh bilioni 40.

Hatua hiyo ya Bunge inafuatia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuzuia makontena 282 yenye mchanga wenye dhahabu katika Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni utekelezaji wa amri ya Rais John Magufuli kuzuia yasisafirishwe kwenda nje ya nchi.

Ndugai alitoa maelezo hayo jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo akitokea mkoani Dodoma akimbatana na wabunge 10 wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Bajeti, ambao walihoji maswali yaliyozaa majibu yaliyotofautiana kutoka miongoni mwa watendaji wa TPA na Wizara ya Nishati na Madini.

Wakati Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko akisema asilimia 90 ya mchanga huo una madini ya dhahabu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justine Ntalikwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Gilay Shamika walimpinga na kueleza kuwa mchanga huo una kiasi kikubwa cha shaba na madini ya fedha.

“Kama mchanga huu una shaba zaidi mbona hakuna hata kontena za Zambia hapa wakati nchi hiyo ndio inazalisha zaidi shaba,” alihoji Ndugai huku Profesa Ntalikwa akitaka ufanyike uchunguzi zaidi kujua ni madini gani yapo kwa wingi katika mchanga huo.

Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, Terminal I, Ndugai alikwenda moja kwa moja bandarini na kufanya kikao cha ndani, kabla ya kuanza kukagua makontena hayo yaliyokuwa yamegawanywa katika maeneo matatu tofauti.

Katika msafara huo, Ndugai na wabunge walishikwa na butwaa baada ya kuelezwa kuwa sampuli ya mchanga huo ikishapimwa na TMAA, hakuna mtu yeyote anayehakiki zaidi ya mgodi husika na nchi unapokwenda.

Siku nne zilizopita Rais John Magufuli alishuhudia makontena 20 katika bandari hiyo yakiwa na mchanga wenye dhahabu, ambapo aliagiza kutosafirishwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama.

Baada ya agizo hilo, juzi yalikamatwa mengine 256 katika bandari hiyo na kufanya idadi yake kuwa 282 baada ya moja kuongezeka jana kwa mujibu wa Kakoko.

Ilivyokuwa

Kakoko: Kontena zote zinapita kwenye skana na kuna skana sita za kukagua kontena zitafungwa. Kwa sasa kontena zote tunazozikamata tunaziweka alama ya X na zipo chini ya ulinzi na hapa kuna kamera tunaona kila kitu kinachofanyika.

Ndugai: Mtu wa TMAA yuko wapi? Hivi kontena ngapi zipo katika mgodi wa Buswagi na Bulyanhulu, ngapi zipo njiani na ngapi zimeshafika hapa Dar es Salaam?

Mhandisi Shamika: Hapa sina takwimu kamili zipo ofisini maana kontena zikisafirishwa mkaguzi wetu anakuwa na takwimu zote.

Ndugai: Kwa wastani mnatoa kontena ngapi kwa mwaka zinazosafirishwa?

Mhandisi Shamika: Kwa mwaka Buzwagi ni kontena 24,000 na Bulyanhulu kontena 21,000. Wastani kwa mwaka zinakuwa kontena 55,000 hadi 60,000 za tani 20 kila moja.

Profesa Ntalikwa: Ili kujiridhisha na taarifa za mali iliyopo kwenye kontena ni kutengeneza timu ya wataalam kuchukua sampuli kupeleka maabara ili kuzipima. Timu hii ihusishe taasisi nyingine, tukimaliza zoezi hilo tutaitoa taarifa ili kila mtu ajue.

Ndugai: Anayepima mchanga huu ni mwajiliwa wa TMAA, hivi kuna mtu mwingine anayepima?

Mhandisi Shamika: Sampuli tunapima sisi TMAA, mgodi wenyewe na pia huko nchi unakokwenda huu mchanga nao wanaupima ili kujiridhisha na vipimo vyetu. Vipimo vyetu hupishana kidogo.

Ndugai: Kampuni za madini zimesajiliwa Uingereza si ndio? Wazungu hao, kontena hizi zinaenda hukohuko kwa wazungu, kwanini wewe TMAA usiwe na watu watatu zaidi ndani yako wa kujiridhisha na vipimo? Hamdhani hawa wazungu wanaweza kukubaliana kutoa takwimu za uongo.

Mhandisi Shamika: Tumelichukua hilo mheshimiwa. Ila dhahabu katika mchanga huu ni asilimia 0.02.

Kakoko: Tuna imani na hatuna wasiwasi kuwa asilimia hizo za dhahabu sio zenyewe. Humu tuna dhahabu nyingi mno asilimia 90. Katibu Mkuu ni mgeni anapokea taarifa tu. Tunataka kupata takwimu za kuanzia Julai, tutawaandikia barua kesho (leo) asubuhi. Hivi mbona TRA hawakagui hapa?

Profesa Ntalikwa: Tunataka usafishaji wa mchanga kufanyika hapa nchini, tunatafuta mwekezi na ni zoezi tunaloendelea nalo ili kupata mwekezaji.

Ndugai: Hivi mtu anaweza kuwekeza eneo la dhahabu lenye asilimia 0.02 kweli?

Mhandisi Shamika: Kwa asilimia hiyo mwekezaji hawezi kuwekeza.

Ndugai: Kama hawezi, iweje achukue asilimia 0.02 ya kiwango cha dhahabu asafirishe na kuingia gharama mpaka Japan (kicheko). Hili tuliache hivi hivi.

Mhandisi Shamika: Shaba ni asilimia 17 na dhahabu ni asilimia 0.02, na madini ya fedha ni 0.02 huyu ni mfanyabiashara anataka kupata vitu vyote vitatu.

Kauli ya Ndugai

“Tukienda bungeni tutatangaza hatua tutakazochukua. Ila kwanza tutaunda timu ya wabunge na itachunguza jambo hili kuanzia mgodini hadi kwenye usafirishaji,” alisema Ndugai.

“Tunataka kujua biashara hii inaendeshwa na nani na nani anayefaidika. Tutataka kujua katika madini watanzania wananufaika vipi maana tangu mwaka 1998 kontena 50,000 zinasafirishwa kwa mwaka kwenda nje.”

Alisema haiingii akilini tangu kipindi hicho hadi sasa kiwango cha dhahabu kinachosafirishwa kiwe asilimia 0.02 katika kila kontena lenye mchanga huo.

“Tutaipitia mikataba ya madini yote ili kujua nini kilichomo humo na tutachukua jukumu la kuishauri Serikali. Tunataka kujua nani anasimamia maslahi yetu huko mchanga unapokwenda,” alisema Ndugai.

Alisema wakati umefika kwa Watanzania kuchukua hatua kwa madai kuwa utajiri wan chi unaondoka kila uchwao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo