Walalamika kunyanyaswa na trafiki


Dalila Sharif

MADEREVA wa daladala zinazofanya safari za Temeke na Muhimbili wameliomba Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Temeke kuwaokoa dhidi ya unyanyasaji wanaofanyiwa na baadhi ya askari wa kikosi hicho wilayani humo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi Dar es Salaam katika barabara ya Kivungo, mtaa wa Kitunda juzi, madereva na makondakta wao walisema wamechoshwa na unyanyasaji wa baadhi ya askari hao,   unaorudisha nyuma maendeleo yao.

Mmoja wa madereva, Awadhi Khalifa alisema baadhi ya askari wamekuwa wakiwabambikizia makosa na kuwanyanyasa wanapokuwa kazini na kutaka Jeshi hilo lirekebishe hali hiyo.

“Tunakamatwa ovyo bila makosa kila siku. Kuna makosa ya ukweli tunajua, lakini mengi ni ya kubambikiwa. Unasingiziwa umefanya kosa hili, tena unaulizwa uandikiwe au ulipe pesa mkononi kwa askari. Hali hiyo tumechoka nayo kwani inaturudisha nyuma katika kazi zetu,” alisema Khalifa.

Akiunga mkono hauli ya mwenzake, Michael Tumaa alisema wamekuwa wakiwachumia pesa askari hao kwani wao hawafaidiki na kazi hiyo.

Alisema: “Kituo cha daladala Chang’ombe husimamishwa na baadhi ya askari hao na kukamatwa kwa kuonekana kuwa eti tumeiba njia, hali ambayo si kweli. Hapo hutozwa faini au wengine kupelekwa kituo cha Polisi,” alisema Tumaa.

Madereva hao walisema ni vema polisi wakazingatia haki katika kazi zao na kuepuka unyanyasaji wa madereva wilayani humo.

“Rushwa pia imetawala kwa baadhi ya polisi, tunahimiza wabadilike na wakubwa wao wafuatilie suala hili,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo