Z'Bar yametimia uanachama CAF


Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar

HATIMAYE Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limeipa uanachama rasmi Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) na kufanya shirikisho hilo kuwa na wanachama 55.

ZFA kwa muda mrefu ilikuwa ikihaha kupata uanachama huo lakini katika Mkutano Mkuu wa CAF uliofanyika jana jijini Adiss Ababa, Ethiopia ulipitisha kwa kauli moja uamuzi huo.

Mkutano huo ambao pia uliambatana na uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo, ulimuingiza madarakani Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Madagascar, Ahmad Ahmad kwa kumpigia kura za ndiyo 34 huku Issa Hayatou ambaye alikuwa akitetea nafasi yake akipata kura 20.

Wadau wa michezo visiwani Zanzibar wakizungumza baada ya ZFA kukubaliwa uanachama, wameielezea hatua hiyo ni miongoni mwa mafanikio na maendeleo ya mchezo huo nchini.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, Kheri Adam Aliy alisema amepokea kwa furaha taarifa hiyo akiamini kuwa maendeleo makubwa yatapatikana katika mchezo huo.

“Hii ni hatua ambayo imehitimisha harakati za muda mrefu. Nawapongeza TFF na ZFAkwa hatua hii ambayo itatoa nafasi kwa wachezaji wengi zaidi kushiriki katika mashindano ya CAF”, alisema mwenyekiti huyo.

Aidha alivitaka vyama vingine vya ngazi ya wilaya kushikamana na kujiandaa kwa mabadiliko yatakayotokana na hatua hiyo na kuwatahadharisha kuwa isiwe chanzo au sehemu ya migogoro isiyo na tija katika soka la Zanzibar.

Pia Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Zanzibar (ZASWA), Donisya Thomas mbali ya pongezi kwa ZFA, aliwataka wadau wa soka nchini kuendelea kushikamana na kustawisha utulivu uliopo katika soka la Zanzibar ili iweze kunufaika na uanachama huo.

“Tusheherekee mafanikio haya tukielewa kuwa kama wadau wa michezo tuna dhima ya kuwasadia ZFA kufikia malengo yake katika sura mpya ya kuwa mwanachama kamili wa CAF”, alisema katibu huyo.

Akizungumzia hatua hiyo, Ofisa Habari wa ZFA, Ali Bakari ‘Cheupe’ aliwashukuru viongozi mbali mbali walioshiriki katika mchakato huo tangu ulipoanza mwaka 2004 na kuyataja mafanikio hayo kuwa ni matunda ya juhudi zao.

Katika hatua nyingine, Ahmad alichaguliwa kuwa rais mpya wa CAF baada ya kupata kura 34 kati ya 54 zilizopigwa huku mpinzani wake, Hayatou akipata kura 20.

Kwa matokeo hayo, yamefuta uongozi wa Hayatou ambaye aliongoza shirikisho hilo kwa miaka 29.

Ahmad amekuwa rais wa saba wa CAF kuongoza shirikisho hilo tangu miaka 60 iliyopita ya kuundwa kwake. Pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limempongeza rais huyo mpya na kuahidi itaendelea kutoa ushirikiano kwa hali na mali katika kukuza soka Afrika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo