Mavugo ‘asepa na kijiji’ Arusha


Mwandishi Wetu, Arusha

Laudit Mavugo
BAO pekee lililofungwa dakika ya 54 na mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo (pichani), limetosha kuipeleka Simba nusu fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya kuichapa Madini FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa.

Kwa ushindi huo, Simba imeungana na Mbao FC ya Mwanza kufuzu hatua hiyo ambayo juzi iliichapa Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Mbali na timu hizo, mabingwa watetezi wa kombe hilo, Yanga itaumana na Prisons ya Mbeya na Azam FC itaoneshana jasho na Ndanda FC katika kuwania kucheza hatua hiyo.

Katika mchezo huo, timu hizo zilianza kwa kasi na kushambuliana kwa zamu ambapo katika dakika 15 za kwanza zilionekana kusomana mchezo.

Dakika ya 22, Madini ilibisha hodi langoni mwa Simba lakini shuti lililopigwa na Razaro Costantine dakika ya 22 liliokolewa na kipa, Daniel Agyei.

Simba ilijibu shambulizi hilo dakika ya 30 kupitia kwa Ibrahim Ajibu ambaye alipiga shuti na mpira kugonga mtamba wa panya na kurudi uwanjani lakini mabeki waliondosha hatari.

Timu hizo ziliendelea kuchezeana ubabe ambapo katika kipindi hicho wachezaji wa Simba, Mzamiru Yassin na Juuko Murshid walioneshwa kadi za njano na kwa Madini ni Awesu Awesu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Simba kufanya shambulizi la nguvu dakika ya 46 kupitia kwa Ajib lakini kipa Cheramanda aliudaka mpira uliopigwa na mshambuliaji huyo.

Simba iliongeza presha langoni mwa Madini na dakika ya 54, Mavugo aliifungia timu yake bao pekee kwa kichwa baada ya beki, Hamis Hamis kuzembea kuondosha hatari langoni mwake.

Timu hiyo iliendelea kutakata ambapo Winga Shiza Kichuya alikosa bao akibaki na kipa Cheramanda baada ya shuti lake kuokolewa na beki Hamis kuondosha hatari.

Pamoja na kufungwa bao hilo, Madini iliendelea kujitutumua hasa alipoingia mshambuliaji mkongwe, Bakari Kigodeko ambaye alionekana kuleta uhai katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa, mashabiki wa Simba walishangilia kwa nguvu na baadaye walionekana wakitaka kuingia uwanjani lakini Polisi walifanya kazi ya ziada kuwazuia hivyo walijikuta wakimfuata Mavugo kwa nyuma.

Simba: Daniel Agyei, Besala Bukungu, Mohamed Zimbwe, Abdi Banda, Juuko Murshid, James Kotei, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin/ Jonas Mkude, Laudit Mavugo, Ibrahim Ajibu/Athanas Pastory na Mohamed Ibrahim.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo