Pigo la tano kwa Dk Mwakyembe


Mwandishi Wetu

Dk Harrison Mwakyembe
SASA ni dhahiri kuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe, anakabiliwa na wakati mgumu wa utekelezaji wa majukumu yake, kutokana na mazingira ya kisiasa yanayomzonga.

Jana katika mfululizo wa majanga ya kisiasa yanayomwandama, Dk Mwakyembe anayejulikana kwa umahiri kwenye sheria nchini, alijikuta katika wakati mgumu pale agizo alilotoa juzi kwa Watanzania, lilipofutwa na Rais John Magufuli.

Kabla ya hatua hiyo ya Rais dhidi ya agizo la mteule wake, Dk Mwakyembe alikuwa katika wakati mgumu wa kisiasa, kutokana na tamko lake lingine la kutishia kufuta usajili wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kupingwa na wanataaluma wenzake.

Juzi Dk Mwakyembe aliagiza kuwa kuanzia Mei mosi viongozi wa Serikali, mila na dini wanaofungisha ndoa wahakikishe kabla ya kufanya hivyo waoanaji wawe na vyeti vya kuzaliwa.

Kupingwa kwa tishio hilo na wanasheria, kulienda sambamba na uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, kuwa miongoni mwa wagombea wa urais wa TLS, jambo lililoonekana kutotiliwa maanani kwa nguvu na ushawishi wa Waziri huyo kwa wanasheria wenzake.

Itakumbukwa pia kuwa Waziri huyo katika sakata la vita dhidi ya dawa za kulevya, alijikuta matatani, pale Rais Magufuli aliposema huenda alidanganywa kuhusu Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, wakati Dk Mwakyembe ni mmoja kati ya washauri wakuu wa Rais katika masuala ya sheria.

Lakini hata uteuzi uliofanyika mwanzoni mwa mwaka huu wa gwiji mwenzake wa sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, kuwa Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, kuliibuka minong’ono ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, huku umahiri wa sheria wa Profesa Kabudi, ukihusishwa na mabadiliko katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Kufutwa agizo
Jana Rais Magufuli alifuta agizo la Dk Mwakyembe siku moja tu baada ya kutolewa la kuwataka Watanzania wote watakaofunga ndoa kuanzia Mei mosi, kuwa na cheti cha kuzaliwa.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa Rais amefuta agizo hilo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi kabla ya kuondoka Ikulu ya Chamwino, Dodoma kurejea Dar es Salaam.

“Dk Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu masharti hayo kutumika, kwa kuwa yatawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji,” ilieleza taarifa hiyo ya Msigwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mpaka sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20, huku wengi wao wakiwa ni waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.

“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania, msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe, nitamwelekeza Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe apelike bungeni kikarekebishwe,” alikaririwa Rais Magufuli na taarifa hiyo.

Aidha, Rais Magufuli alitoa mwito kwa Watanzania kuendelea kupata vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na kutaka viongozi wote kuhamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo.

Tishio la TLS
Rais Magufuli alifuta agizo la Mwakyembe, wakati Waziri huyo akijadiliwa katika majukwaa ya kisheria na kisiasa, kutokana na kauli yake ya kutishia kufuta Sheria ya TLS Sura ya 307 iliyoanzisha chama hicho.

Dk Mwakyembe akizungumza na ugeni wa TLS uliomtembelea ofisini kwake Dodoma ukiongozwa na Rais wao, John Seka, alikaririwa akisema kuwaingiza wanachama wenye nasaba za siasa au viongozi wa vyama vya siasa ndani ya TLS, ni kuruhusu mgongano wa maslahi na yeye ni mwanasheria hivyo hawezi kukubali jambo hilo.

“Wizara hatujui mwelekeo wa TLS kwa sasa, hatuwezi kuiacha TLS ikijiingiza katika siasa halafu tukawaangalia tu. Hatuna nia ya kuitawala TLS, ila tunawajibika kuwasimamia kwa kuwa sheria yenu iko chini yetu.

“Mkiharibu kwa lolote, Wizara ndiyo yenye wajibu wa kuwatolea maelezo na katika hilo mnalotaka kulifanya sasa, kuna mgongano wa maslahi, je ninyi kama wanasheria hamkuliona au hamlioni?” Alihoji Mwakyembe.

Mbali na wanasheria kadhaa kumpinga kwa kauli hiyo, Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS), kilimwandikia barua ya wazi Mwakyembe, iliyosainiwa na Rais wake, Richard Mugisa kumtaka aache kuingilia uchaguzi wa TLS.

Barua hiyo iliungwa mkono na TLS, pale Seka alipoeleza kufurahishwa kwake na barua hiyo na kufafanua kuwa chama hicho kilikuwa mbioni kukutana na Mwakyembe ili kujadili mustakabali wa chama hicho.

Mgombea TLS
Kama haitoshi, Lissu na kada mwingine wa Chadema, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha walithibitishwa kuwa wagombea urais wa chama hicho, kinyume na maoni ya Dk Mwakyembe na Rais Magufuli kuhusu wanasiasa na chama hicho.

Wengine walioidhinishwa kugombea nafasi hiyo ni pamoja na aliyewahi kuwa Rais wa TLS, Francis Stola, aliyewahi kuwa mgombea urais kupitia CCM mwaka 2015, Godwin Mwapongo na Wakili Victoria Mandari.

Mbali na kuthibitishwa kuwa wagombea katika uchaguzi unaofanyika leo, lakini hata kesi mbili zilizofunguliwa Mahakama Kuu Dodoma na Dar es Salaam kupinga uchaguzi huo, zilitupwa zote juzi.

Kesi ya Dodoma ilifunguliwa na Wakili Godfrey Wasonga, akipinga uchaguzi huo akidai kuwa kanuni za uchaguzi huo ni batili; huku ya Dar es Salaam ikifunguliwa na Wakili Onesmo Mpinzile, dhidi ya TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nayo dhidi ya kanuni hizo za uchaguzi.

Kufichwa sheria
Mwakyembe alijikuta katika wakati mgumu katika sakata hilo la TLS, siku chache baada ya Rais Magufuli kutamka wazi kuhusu uwepo wa njama za kumficha Sheria ya Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya mwaka 2015.

Akizungumza Ikulu Dar es Salaam Februari 12, Rais Magufuli alisema Waziri Mkuu na mawaziri walifichwa sheria hiyo na hata Waziri Mkuu alifichwa kwamba yeye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Kupambana na Dawa za Kulevya.

“Waziri Mkuu mwenyewe alijua jana au juzi kwamba ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo,” alibainisha Rais Magufuli. Alisema hana uhakika kama mawaziri husika kwenye Baraza hilo walikuwa na taarifa ya kuwa wajumbe, maana walifichwa na wasaidizi wao wizarani, hadi walipoelezwa na Waziri Mkuu kwamba wanawajibika kupambana na dawa za kulevya.

Rais Magufuli alisema kutokana na ugumu uliopo hata ndani ya Serikali, ndiyo maana hakuwahi kupelekewa jina ili ateue Kamishna wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, hadi alipoamua mwenyewe kumteua kwa njia alizozijua.

“Nilikuwa najiuliza kwa nini sijaletewa mapendekezo ya uteuzi wa Kamishna wa Dawa za Kulevya, baada ya kuona kimya nikaamua kuteua mwenyewe, kwa hiyo mnaona vita hivi vilivyokuwa vikubwa, ndani ya Serikali si malaika,” alikaririwa Rais.

Kabudi
Januari Rais Magufuli aliteua wabunge wawili, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo na nguli wa sheria, Profesa Kabudi, ambaye alihusishwa moja kwa moja na uwezekano wa mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Katika mtazamo huo, Profesa Kabudi kwa weledi wake alihusishwa na mabadiliko katika Wizara ya Katiba na Sheria, inayoongozwa na Dk Mwakyembe.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alikaririwa akisema: “Siwezi kuwa mtabiri, lakini ukisoma alama za nyakati na uteuzi huu kufanyika sasa, inawezekana si wote, lakini nafikiri anaweza (Rais Magufuli) kufanya mabadiliko katika Baraza lake.

“Mfano Profesa Kabudi ni mzoefu, msomi na anaijua Tanzania. Ana uwezo mkubwa wa kujieleza na kujenga hoja. Sidhani kama Rais atamwacha hivi hivi akiwa mbunge tu.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo