Wachimbaji wadogo madini wamlilia JPM

Fidelis Butahe

Rais John Magufuli
UAMUZI wa Rais John Magufuli kuzuia mchanga wa dhahabu kusafirishwa nje ya nchi umewaathiri wachimbaji wadogo.

Wachimbaji hao jana walimpigia magoti Mkuu huyo wa Nchi wakieleza kuwa hali hiyo imesababisha wapate hasara, huku mamia ya wananchi wakikosa ajira.

Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, wachimbaji hao sita wa madini ya aina mbalimbali waliozungumza kwa niaba ya wenzao, walisema licha ya lengo zuri la Rais, uamuzi wa kuwabana hata wao ambao hawachimbi   dhahabu lakini wanasafirisha mchanga wenye madini mengine, unapaswa kuangaliwa upya.

Kwa mujibu wa wachimbaji hao, hadi jana kontena zao zaidi ya 60 zimezuiwa maeneo mbalimbali nchini huku wakilazimika kulipa Sh 45,000 kwa siku kwa kila kontena, huku wakishauri yaachwe hayo pamoja na yaliyoko bandarini ili kusaidia wasipate hasara.

Hadi Jumapili kontena 282 zenye mchanga wa dhahabu zilikuwa zimezuiwa kwenye bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni takribani siku tano tangu Rais Magufuli ashuhudie kontena 20 zenye mchanga huo.

Rais alizuia kusafirishwa kwa mchanga huo na kuwekwa chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama katika hatua ambayo Bunge liliingilia kati na kuunda timu ya uchunguzi wa biashara ya madini nchini, huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa uteuzi wake ukitenguliwa.

“Mimi ni mchimbaji na msafirishaji  wa madini ya nikeli. Nimeathirika na zuio la Rais Magufuli kwa sababu nimesimamisha shughuli zangu na kusitisha ajira kwa wachimbaji wangu.

“Kifupi nimefilisika maana kontena zangu 13 ilikuwa nizisafirishe nimeshindwa bado ziko mgodini  Mpwapwa, Dodoma, “ alisema Thobias Rweyemamu, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini ya Metali.

Rweyemamu alisema akisitisha shughuli mgodini mwake kwa siku moja anaingia hasara ya Sh milioni 4, na sasa amesitisha uchimbaji kwa takribani mwezi mmoja.

King Seleman ambaye anachimba madini ya metali pekee alisema, “migodi mingi tunayopata kutoka wizara ya madini ni ya shaba na kutokana na kiwango kidogo cha madini hayo na mengine, ndiyo maana hakuna mwekezaji anayeweka kiwanda.”

Alisema wenye migodi ya dhahabu wanafaidika kwa sababu huambatana na madini ya shaba na fedha na kusisitiza kuwa wanapozuiwa kusafirisha mchanga wenye shaba na madini mengine wanaathirika huku akidai zuio la Rais linahusu wachimbaji wakubwa.

“Sisi ni wamachinga katika sekta ya madini. Ni kama wamachinga walio Kariakoo. Rais atufikirie,” alisema.

Mohamed Mkwayu ambaye ni mchimbaji mdogo wa shaba alisema, “zuio linakosesha wafanyakazi mshahara na sisi tumesitisha kuchimba maana hakuna pa kuupeleka mchanga. Rais ametuumiza kwa kweli, sisi tunachimba shaba si dhahabu.”

Paul Kalyembe anayechimba shaba, garena na zinki alisema wanalipa leseni ya Sh milioni 14 kuchimba madini hayo, tayari wameshalipa na kumtaka Rais alegeze uamuzi wake.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo