ACT-Wazalendo wamkumbusha Rais JPM Katiba Mpya


Abraham Ntambara

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimemtaka Rais John Magufuli kuendeleza Mchakato wa Katiba Mpya kwa kuanzia ilipoishia Rasimu ya Pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa ACT, Msafiri Mtemelwa alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.

Alimtaka Rais Magufuli kuendeleza mchakato huo hadi Katiba hiyo mpya itakapokamilika. “Rais Magufuli aanze na Rasimu ya Jaji Warioba iliyokuwa inatoa nguvu kwa wananchi kuwawajibisha viongozi wao pale wasipotekeleza wajibu wao kulingana na nafasi walizonazo,” alisema Mtemelwa.

Alisema kwa namna wanavyomfahamu Rais Magufuli ambaye amekuwa akijinasibu kuwa Rais wa wanyonge, wanaamini hatalinda maslahi ya chama chake CCM pekee, bali atawapatia Watanzania Katiba bora kwa maslahi ya Taifa.

Kwa mujibu wa Mtemelwa, Katiba bora itamnufaisha kila Mtanzania na akawaomba viongozi wa dini na taasisi mbalimbali kulitilia mkazo suala hilo ili Katiba Mpya yenye kukidhi kiu na matakwa ya wananchi.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu mkuu huyo wa ACT alisema chama hicho jana kilianza kutoa fomu kwa wanachama wanaohitaji kugombea nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) na kuwataka wanachama wenye sifa wajitokeze.

Alieleza kuwa mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo ndani ya chama utakamilika Machi 21 mwaka huu saa 10:00 jioni ambapo alisema kwa wanachama wa Dar es Salaam watachukua fomu hizo Mako Makuu ya ACT huku walio mikoani wanatakiwa kuwasiliana na Afisa Mawasiliano.

Alisema maandalizi ya mkutano mkuu wa kidemokrasia wa ACT yamekamilika kwa zaidi ya asilimia tisini ambapo watakuwa na mijadala mbalimbali kutoka kwa wawakilishi wa taasisi za ndani na nje.

Alisema mkutano huo utawashirikisha wanachama na wasio wanachama huku ukiwa hauna wajumbe Mahususi ambapo utajikita zaidi katika masuala ya maendeleo ya nchi na dunia kwa jumla.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo