Makonda ashindwa kukata kiu ya vyeti


*Ajikita katika kuendeleza vita vya mihadarati
*Aonya walio mabondeni wahame mara moja

Mwandishi Wetu

Paul Makonda
HAJAKATA kiu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kushindwa kuwajibu baadhi ya watu wanaomtuhumu kutumia cheti cha kidato cha nne cha mtu mwingine kuendelea na elimu ya juu, hatimaye kufika chuo kikuu.

Akizungumza jana katika hafla fupi ya kutimiza mwaka mmoja tangu ateuliwe na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo, Makonda alijikita zaidi kuzungumzia vita dhidi ya dawa za kulevya, mambo aliyoyatekeleza katika kipindi hicho, matarajio yake na mikakati yake mwaka huu, bila kugusia chochote juu ya tuhuma hizo.

Kushindwa huko kwa Makonda kumekuja takribani mwezi mmoja tangu kuanza kwa tetesi za tuhuma hizo na gazeti hili kuziripoti kwa mara ya kwanza Februari 22 na kisha kuzagaa kwenye mitandao ya kijamii huku Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akidai kupata ushahidi wote wa Makonda kutumia cheti cha mtu mwingine.

Makonda ambaye alitumia takribani dakika 70 kueleza masuala mbalimbali katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay na kuhudhuriwa na watu mbalimbali, Makonda alisema hatishwi na kelele zinazoendelea bila kufafanua kama ni tuhuma hizo au la.

“Sitishwi na kelele zinazoendelea…, mwaka wangu wa pili kama Mkuu wa Mkoa nitaongeza kasi mara mbili zaidi katika vita vya dawa za kulevya,” alisema.

Wakati akieleza hayo, taarifa zilizolifikia gazeti hili zilidai kuwa kampuni moja kubwa itasafirisha wanahabari 10 kwenda kijiji cha Kolomije wilayani Misungwi mkoani Mwanza, alikozaliwa Makonda, ikielezwa lengo ni kusaka taarifa za kuzima tuhuma hizo.

Habari hizo zinaeleza kuwa safari ya timu ya wanahabari hao kutoka vyombo mbalimbali vya habari itafanyika wiki hii ambako wameandaliwa wazee wa kuzungumza nao kijijini hapo.

“Baadhi ya wazungumzaji ni walimu wa shule aliyosoma Makonda na wazee wa kijiji hicho,” zilieleza habari hizo.

Licha ya kutogusia elimu yake, Makonda alitumia halfa hiyo, kutaka wazazi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwenye vita hivyo kwa kufuatilia nyendo na tabia za watoto wao na kutoa taarifa katika vyombo vya Dola, ili kusaidia kutimiza ndoto na malengo yao.

“Akina mama mliobeba mimba kwa miezi sita, tunaomba mtuunge mkono ili mateso mliyopata kwa miezi tisa, wengine mlikataliwa, wengine mlikosa hata fedha ya kutunza mimba, wengine mlikatisha masomo yenu na wengine kupewa majina ya hovyo, tunaomba mumuunge mkono Rais John Magufuli katika mapambano ya dawa za kulevya,” alisema Makonda.

Alitaka wazazi kutoacha ndoto za watoto wao ambao waliwalea kwa mateso zipotezwe na wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambapo aliwaomba kufuatilia nyendo za watoto wao.

Aidha, alisema ana taarifa za wanafunzi kujihusisha na matumizi ya dawa hizo akieleza kuwa wanatarajia kuendesha operesheni katika shule za mkoa huo.

Alisema kuna tabia ya baadhi ya wanafunzi kutumia dawa hizo vyooni na kasha kuingia darasani.

Aliongeza kuwa kuna watu wamekuwa wakitumia watoto wadogo wanaotumia dawa za kulevya katika matukio mbalimbali ya wizi na ubakaji.

Mkuu wa Mkoa alisisitiza kwa kuwaambia wazazi wasiwe wa kuamka na kwenda kazini tu pia wawe wanafuatilia mienendo na tabia za watoto wao kwani huwa wanavutishwa bangi, heroin na kokeni na kisha kupewa maelekezo ya kufanya uhalifu.

Alisema wanapoona nyendo wasizozielewa waripoti Polisi ili Serikali iwasaidie kama ambavyo imekuwa ikisaidia wengine na kufafanua kuwa asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na dunia.

Aidha, alisema ni wajibu wa viongozi wa dini kwa mamlaka waliyopewa na Mungu kujisikia vibaya kuwa na waumini wanaoharibika kwa kukemea maovu hayo kwa waumini wao ambapo aliwataka kuwa mstari wa mbele kwenye vita hivyo.

Aliwataka wakazi wa Dar es Salaam, kujua kuwa vita hivyo vinatokana na mapenzi waliyonayo kwao na kukanusha, kwamba hawafanyi kwa lengo la visasi ambapo alifafanua kuwa ndiyo sababu ya kufanya hivyo ili kuhakikisha wananchi wanatimiza ndoto zao.

Kwa upande mwingine, alitaka wakazi wa mabondeni kuondoka kwani mazingira hayo ni hatarishi kwa usalama wao.

Makonda alisema atawapa viwanja wakazi wote wenye hati wanaoishi maeneo hayo hatarishi na kwamba pamoja na kuwapa viwanja, Serikali ya mkoa itashughulikia watumishi waliotoa hati hizo huku wakijua maeneo hayo hayaruhusu makazi ya watu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo