Jeshi la SADC lamwaga ajira


Hussein Ndubikile

JUMUIYA ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) imehamasisha raia wao wenye taaluma na wasionazo kujisajili ili kupata fursa za kujiunga na Jeshi la Ulinzi wa Amani la Jumuiya hiyo.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Msajili na Mkufunzi  wa SADC, Eliet Magogo, katika warsha ya mafunzo ya kuhamasisha raia kujisajili na Jeshi hilo.

Alisema kutokana na mwamko mdogo wa raia wa nchi za SADC kujisajili, Jumuiya imeanza mafunzo kwa maofisa wa taasisi za Serikali lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watakaojiunga.

"SADC inaendesha warsha kwenye nchi wanachama na usajili ukienda vizuri itapata watu wengi watakaohudumia Jeshi hili," alisema Magogo.

Alisema waombaji wenye taaluma watatakiwa kuwa na elimu ya Shahada na uzoefu wa miaka saba ya taaluma yao, huku akiongeza kuwa suala hilo halizuii raia wa kawaida kujisalili kwani ndani ya Jeshi hilo kuna wigo mpana wa majukumu.

Aliongeza kuwa waombaji watafanyiwa mchujo kwa kufuata vigezo vilivyowekwa na watakaofanikiwa kuchaguliwa watapelekwa Chuo cha Mafunzo nchini Zimbabwe.

Alisisitiza kuwa katika Jeshi hilo watu wenye taaluma za udaktari, uhasibu, ukaguzi wa hesabu, uhandisi, uanadiplomasia na wa mawasiliano ya umma wanahitajika.

Alifafanua kuwa kwa wanaotaka kujiunga na Jeshi hilo waingie kwenye mtandao wa SADC ili kupata maelekezo na vigezo vinavyotakiwa.

Pia alisema raia watakaochaguliwa na kupewa mafunzo wataitwa kujiunga na Jeshi endapo watahitajika na kupelekwa nchi zitakazokuwa na matatizo ya usalama.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo