Muhongo azindua mradi wa REA III


Mwandishi Wetu
Profesa Sospeter Muhongo

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amezindua Mradi wa Umeme Vijijini (REA) Awamu ya Tatu mkoani Pwani akisema mkoa huo utapewa kipaumbele kwa kuwa ni kimbilio la wawekezaji na ukanda wa viwanda.

Aidha, ametaka Watanzania kuacha kujidharau kupitia mradi huo kwa kuwa ni mkombozi wao kwani mwaka 2007 kulikuwa na asilimia mbili pekee ya watumiaji nishati ya umeme lakini sasa kasi imefikia asilimia 49.5.

Akizindua mradi huo juzi na kumtambulisha mkandarasi kutoka Tunisia kampuni ya Steg, alisema ni wakati wa kuchangamkia fursa hiyo kwa kila Mtanzania mwenye mahitaji ya umeme.

Alisema katika awamu hiyo, zimetengwa Sh trilioni moja ambapo vijiji 3,559 vitafikiwa nchini huku Pwani ikifikiwa vijiji 150 vilivyokuwa havijafikiwa na awamu ya kwanza na ya pili.

Alisema malengo yao ni kuhakikisha wanafikia vijiji vyote 12,268 nchini, kwa umeme wa Tanesco ili kila mmoja anufaike nao na kuondokana na vibatari.

Profesa Muhongo alisema wakati mradi huo wa REA ukianza katika maeneo mbalimbali nchini ni lazima upelekwe katika zahanati, shule na vituo vya dini.

Alisema mkoa wa Pwani ni kati ya iliyojikita kwenye viwanda na uwekezaji hivyo ni lazima nguvu kubwa ielekezwe huko.

Profesa Muhongo aliutaka uongozi wa mkoa wa Pwani kuweka tayari wataalamu wake na wa Tanesco, REA, wabunge na Meneja wa Kanda, ili kubainisha mahitaji yatakayorahisisha kufanyiwa kazi na wizara.

Alisema fedha zilizotengwa ambazo ni karibu Sh trilioni moja zilizotengwa kwa ajili ya mradi huohazitakuwa sehemu ya fidia kwa ajili ya maeneo ambayo umeme huo utapita.

Aliupongeza uongozi wa mkoa wa Pwani, kwa kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji, pamoja na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete na wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa kwa kupigania maendeleo ya majimbo yao.

Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo alisema mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya wateja na kuomba uongezwe nguvu ya umeme wa megawati 60 ambapo kwa sasa unapata megawati 38 hadi 40 ambazo hazikidhi mahitaji ikizingatiwa kuwa mkoa unasheheni viwanda.

Ridhiwani alieleza mahitaji ya umeme kuwa ni makubwa kwenye vijiji vya Chalinze na kuomba mahitaji mapya yaingizwe kwenye bajeti kwa lengo la kufanyiwa kazi katika bajeti ya mwaka 2017/18.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo