‘CUF’ yajitoa kujibizana na Lipumba


Suleiman Msuya

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimesema hakina muda wa kujibizana na Profesa Ibrahim Lipumba, kwa madai kuwa kundi analoongoza ni la wahuni.

Aidha, CUF imesema hakuna kikao chenye mamlaka ya kumfukuza au kumwondoa madarakani Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad tofauti na mkutano mkuu wa chama hicho.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro wakati akizungumza na JAMBOLEO jana, ikiwa ni siku chache baada ya Lipumba kutangaza kuwa Baraza Kuu la Uongozi la Chama hicho, limekubaliana kumkaimisha Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya nafasi ya Seif.

Alisema wao chama hawana muda wa kukaa na kujadili uamuzi wa kundi la watu ambao alidai ni wahuni hivyo bado wanatambua kuwa Maalim Seif ndiye Katibu Mkuu wao.

Mtatiro alisema Lipumba na kundi lake walishafukuzwa CUF hivyo wanachokifanya kwa sasa hakina tija kwa chama wala kwa wanachama wao.

Mwenyekiti huyo alisema ni aibu kutangaza kuwa Baraza lilikaa na kumteua Sakaya kuwa Katibu wakati hakuna mabaraza mawili ndani ya chama hicho.

“Wakati mwingine ukimwangalia Lipumba na kundi lake, anaonekana amechanganyiwa kinachomlinda ni nguvu ya Dola kumlinda kwani sisi tunawaona ni wahuni fulani ambao wanapingana na ukweli,” alisema.

Mtatiro alitoa mwito kwa wanachama wa CUF kuendelea kushikamana na kuachana na propaganda za Lipumba na kundi lake, kwani hazina nia njema katika chama.

“Sisi hatumtambui Lipumba kama kiongozi wala mwanachama wa chama chetu, hivyo lolote ambalo linafanyika kupitia wao hatuna kazi nalo ni kupoteza muda,” alisema.

Kuhusu mgombea wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), alisema wao wametekeleza agizo la Bunge na kupeleka mgombea mmoja, hivyo iwapo hao wa Lipumba watapitishwa si jukumu lao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo