Simba SC kuzifungia kazi Mbao FC, Toto


Charity James

TIMU ya Simba SC, imesema ipo katika mpango wa kuhakikisha inavunja rekodi katika viwanja vya mikoani ambavyo wamekuwa wakishindwa kupata matokeo mazuri lengo likiwa ni kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kutwaa ubingwa.

Simba inatarajia kushuka uwanjani Aprili 2, mwaka huu kuumana na Mbao FC ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kisha kucheza na Toto Africans.

Katika miaka ya hivi karibuni, Simba imekuwa haina matokeo mazuri ukanda huo hasa katika mechi zake inazocheza Kirumba na Toto African imekuwa ndio kikwazo kwa timu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jackson Mayanja, alisema wao wamekusudia kutwaa ubingwa msimu huu, hivyo wapo tayari kung’oa visiki vyote ili kuhakikisha wanafanya vizuri.

“Tumechoka kuendeleza uteja katika viwanja vyote ambavyo tumekuwa tukipoteza alama muhimu, hivyo hatuko tayari kupoteza ubingwa tunaoutamani kwa muda kisa kupoteza alama nyingi Kanda ya Ziwa,” alisema.

Akizungumzia mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Madini FC ambapo waliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Laudit Mavugo, alisema wanawashukuru wachezaji kwa kufanya kile walichotumwa na mwalimu na kuisaidia timu kuingia katika hatua ya nusu fainali.

Alisema kumekuwa na maneno mengi kuwa safu yao ya ushambuliaji ni butu na kusababisha kupata mabao machache katika michezo yao mbalimbali, kikubwa nni kupata ushindi kwanza na kupata idadi kubwa ya mabao hiyo ni kazi nyingine.

“Ligi ilisimama kwa muda na inatarajiwa kuanza, hivyo mashabiki na wapenzi wa Simba wasife moyo na washambuliaji wetu wapo katika nafasi nzuri ya kufunga idadi kubwa ya mabao na yataweza kutusaidia kuhakikisha tunatwaa ubingwa kama tulivyojipangia,” alisema.

Alisema wapinzani wao wasitarajie kuwa idadi kubwa ya mabao waliyonayo ndio itawasaidia kutwaa ubingwa msimu huu wao bado wana nafasi ya kuongeza idadi ya mabao hayo na pia katika suala la alama kwao haliwapi tabu kwasababu wana imani ya kufanya vizuri katika michezo iliyobaki.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo