Rugimbana ataka vyuo vitoe ushirikiano


Mwandishi Wetu

Jordan Rugimbana
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, amezikumbusha taasisi za elimu ya juu nchini
kuhakikisha zinaongeza uwezo wa madawati ya mikopo yaliyopo katika taasisi zao ili yaweze kutoa ushirikiano unaotakiwa kutatua changamoto za utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Mkuu wa mkoa huyo alitoa agizo hilo jana, wakati akifungua mkutano wa kazi wa siku mbili wa watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), na maofisa mikopo zaidi ya 100 kutoka taasisi za elimu ya juu nchini wanaokutana katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

“Majukumu ya bodi ni mazito na hivyo, inahitaji ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau mbalimbali mkiwemo maofisa mikopo mliopo vyuoni na mnaokutana na wanafunzi kila siku,” alisema Rugimbana, katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi (Elimu) wa Mkoa wa Dodoma, Gosbert Damazo.

Akizungumza katika mkutano huo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema bodi yake inatambua mchango mkubwa unaotolewa na maofisa mikopo hao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu waliopo katika taasisi mbalimbali.

“Maofisa hawa ndiyo wanaotuunganisha na wanafunzi katika utendaji kazi wetu wa kila siku, hivyo ni watu muhimu sana kwetu na tunathamini sana mchango wao na wa taasisi zao,” alisema Badru.

Kwa mujibu wa Badru, bodi yake itatumia mkutano huo wa siku mbili kuwakumbusha maofisa hao wajibu wao katika kutunza kumbukumbu muhimu za wanufaika wa mikopo na majukumu yao muhimu ili kuongeza ufanisi na hivyo kupunguza malalamiko ya wadau wakiwemo wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu.

Mkurugenzi mtendaji huyo alikumbusha kuwa, mwaka 2011, serikali ilivielekeza vyuo vyote vya elimu ya juu nchini kuanzisha madawati ya mikopo ya elimu ya juu ili kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na serikali.

“Tangu mwaka 2011, kumekuwa na mafanikio makubwa katika utendaji wetu kutokana na kuongezeka kwa ufanisi. Hivi sasa malalamiko kutoka kwa wanafunzi
yamepungua sana,” alisema Badru.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Taaluma), Profesa Lawrence Msoffe ambaye alihudhuria hafla ya ufunguzi, alisema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa utaisaidia bodi kupata mrejesho kutoka kwa maofisa hao ambao ndiyo wanaosimamia masuala ya utoaji mikopo katika vyuo kila siku.

HESLB ilianzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi Julai 2005, pamoja na mambo mengine, kutoa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi Watanzania wasio na uwezo na kukusanya mikopo iliyoiva iliyotolewa na serikali kuanzia mwaka 1994/1995.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo