Halmashauri Mbozi yakumbwa kashfa


Ibrahim Yassin, Mbozi
 

Chiku Galawa
TUME ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Chiku Galawa, iliyoundwa kuchunguza ubadhirifu wa Sh milioni 410 za ruzuku kutoka serikalini kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, imebaini ubadhirifu na kuagiza wahusika wahojiwe na kushitakiwa.

Serikali Kuu ilitoa fedha za ruzuku kwa ajili ya shughuli za maendeleo wilayani humo mwaka 2011/12 ambazo zinadaiwa kutofanya shughuli kusudiwa na kuingizwa kwenye akaunti isiyo ya Halmashauri na kutumika vibaya.

Wakati fedha hizo zikiingia, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo wakati huo alikuwa Levson Chilewa na Mwenyekiti wa Halmashauri Erick Ambakisye ambaye hadi sasa anaendelea na wadhifa huo.

Fedha hizo zilizua utata mkubwa huku madiwani wakihoji matumizi yake ambapo Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alibaini kuwapo ubadhirifu huo.

Mwaka jana, Galawa aliunda tume kubaini utata huo baada ya malalamiko ya madiwani ikabaini ubadhirifu na kuamuru wahusika hata kama walistaafu waitwe kuhojiwa, kisha kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumzia hali hiyo jana, Galawa alitaja wahusika wakuu kuwa ni Chilewa ambaye amestaafu, Mganga Mkuu (DMO) Charles Mkombachepa, Ofisa Mipango, Christopher Nyalubamba, Ofisa Elimu Sekondari, Isaack  Mgaya na Mhazini Mkuu, Rashid Mbegumoja.

Galawa alisema baada ya tume kukamilisha uchunguzi ilibainika fedha hizo kupelekwa kwa wakuu wa idara na kuamua waitwe kuhojiwa kisha wachukuliwe hatua stahiki  na mwajiri wao ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Edina Mwaigomole ambaye yuko likizo ya kustaafu aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu, kuwa alipelekwa kufanya kazi kwenye Halmashauri hiyo mwaka 2014 ambako alikuta tuhuma hizo huku akiwa hana mawasiliano na mtangulizi wake, Chilewa.

Wananchi walisema Halmashauri hiyo imekuwa na kashfa nyingi za ubadhirifu wa fedha za maendeleo, hali inayosababisha kupata hati chafu zenye shaka kwa zaidi ya miaka minne mfululizo, wakihimiza hatua zichukuliwe haraka au Halmashauri hiyo ifutwe kuliko kugeuzwa ‘shamba la bibi’.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo