Mgeja amvaa Profesa Kabudi


Hastin Liumba, Kahama

Profesa Palamagamba Kabudi
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyeteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli ameombwa kuanza kazi yake kwa kufufua ajenda ya Katiba Mpya inayogusa maslahi mapana ya Taifa.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation, taasisi inayoshughulikia utawala bora na haki, Khamis Mgeja wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani hapa juzi kuhusu mustakabali wa Taifa.

Alisema suala la Katiba Mpya si la kikundi, wala mtu hivyo akashauri mawazo ya wananchi yaheshimiwe.

“Namtambua Profesa Kabudi kuwa ni msomi aliyebobea katika sheria, tunamwomba uzoefu wake wa masuala ya sheria amshauri kwa umakini Rais Magufuli kuhusu matakwa ya wananchi ya kupata Katiba mpya,” alisema.

Alisema ni vema Waziri akatumia fursa hiyo kumshauri Rais Magufuli kuhusu Katiba Mpya sasa ili mchakato wa kupatikana kwake uanze tena na hatimaye ufikie tamati.

Mgeja alisema bahati nzuri Profesa Kabudi alikuwa mmoja wa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba na kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu iliyotokana na matakwa na maoni ya wananchi.

“Waziri atumie fursa hiyo na tuna imani suala hilo la Katiba Mpya sasa kama ni upele umepata mkunaji,” alisema Mgeja.

Hata hivyo, aliihadharisha Serikali isije kutafuta visingizio katika kutekeleza suala hilo na kwamba shaka yao ni visingizio kuwa muda hautoshi kufanya mchakato wa Katiba Mpya.

Mgeja alisema zaidi ya Sh bilioni 300 zilitumika kwenye mchakato huo na ikiwa hakuna umuhimu wa suala hilo, fedha hizo zingetumika katika huduma zingine za jamii kama afya, maji, ujenzi wa miundombinu au kununua chakula cha akiba na njaa.

Aliikumbusha Serikali ya Awamu ya Tano kwamba suala hilo la Katiba Mpya lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/20 na chama hicho kimeingia mkataba na Watanzania kuwaongoza, hivyo wana deni kubwa kwa wananchi kuwapa Katiba Mpya.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo