Wenye kontena za mchanga watakiwa kujenga mtambo


Mwandishi Wetu

Kassim Majaliwa
SERIKALI imeitaka kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu kujenga mtambo nchini kwa ajili ya uchenjuaji dhahabu.

Nia ni kupunguza malalamiko ya wananchi kuwa madini hayo yamekuwa yakiibwa kupitia mchanga unaosafirishwa. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa rai hiyo jana alipofanya ziara ya kushitukiza kwenye mgodi wa dhahabu wa Buzwagi iliyodumu saa moja na kujionea shughuli za uzalishaji kwenye mgodi huo mjini Kahama. 

Alisema Watanzania hawaamini kama mchanga huo una madini ya dhahabu na shaba.

“Tunataka mjenge mtambo wa uchenjuaji madini ya dhahabu nchini ili kujiridhisha na mapato yatakayotokana na shughuli mnazofanya kupitia kodi stahiki ambayo mtakuwa mkilipa serikalini kwa mujibu wa sheria,” alisema Majaliwa. 

Aliongeza kuwa kwa sasa Serikali itakaa na wawekezaji hao kuona mchakato wa jinsi ya Acacia watakavyojenga mtambo huo na kuondoa lawama za Watanzania kuwa madini hayo yamekuwa yakiibwa.

Aidha, Majaliwa alisema wazekezaji hao kama watajenga mtambo huo nchini, Serikali itapata mapato makubwa zaidi   hali ambayo itasaidia ukuzaji wa uchumi kutokana na kodi stahiki ambayo italipwa nao. 

Waziri Mkuu alisema moja ya makubaliano ya wawekezaji hao na Serikali tangu mwaka 2009 ni kujenga kiwanda cha uchenjuaji madini nchini.

Alisema wawekezaji hao wakijenga mtambo huo nchini pia wataongeza ajira kwa Watanzania wengi huku akiisisitiza kampuni hiyo kutopunguza wafanyakazi kutokana na Serikali kuzuia usafirishaji wa kontena zao za mchanga wa dhahabu kwenda nje. 

“Kwa sasa nimekuja kuangalia uzalishaji wa dhahabu na kontena zilizo kwenye mgodi wenu na kuchukua sampuli ya mchanga unaosadikiwa kuwa asilimia 50 yake ni madini ya dhahabu na asilimia 50 nyingine ni madini mengine ambayo ni shaba,” alisema Waziri Mkuu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo