Mfuko wa Bima ya Afya wapuuza taarifa


Mary Mtuka

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umetaka Watanzania kupuuza taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Mfuko huo uko hoi kiasi cha kushindwa kutoa huduma kwa wanachama wake.

Akikanusha madai ya taarifa hizo za upotoshaji Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bernard Konga alisema taarifa hizo ni upotoshaji wa hali ya juu na ni vema zikapuuzwa huku akiwahakikishia Watanzania kuwa Mfuko uko imara na unatoa huduma kama kawaida.

Alifafanua kuwa taarifa hizo zilianza kutolewa na mtandao wa kijamii wa Jamii Forums na kusambaa kwenye mitandao mingine.Taarifa hiyo ya upotoshaji ilikuwa inadai hivi: "NHIF hoi, watunga muswada kuinusuru, mashirika makubwa kama Tanesco, BoT, TRA, TPA, kujiunga kwa lazima.

"Taarifa hiyo si ya kweli na imejaa upotoshaji kwa umma.Tunaomba mzipuuze, Mfuko wetu uko imara na unaendelea kutoa huduma kama kawaida yake," alisema.

Akijibu hoja ya kwamba Mfuko uko hoi na umeshindwa kuwalipa watoa huduma wake, alisema si za kweli na mtandao huo ulikuwa na lengo la kupotosha umma.

Kuhusu madai ya ucheleweshaji ulipaji madai kwa kukosa fedha na kusababisha wanachama kunyimwa huduma, alisema kwa mujibu wa sheria  ya Mfuko, malipo kwa watoa huduma waliosajiliwa yanatakiwa kulipwa ndani ya siku 60 tangu kuwasilishwa kwake na lengo la kufanya hivyo ni kuhakiki uhalali wa madai yaliyowasilishwa.

Akizungumzia madai ya wigo mdogo wa huduma zitolewazo kwa wanachama, alisema Mfuko umeendelea kufanya maboresho kwenye kitita cha mafao yatolewayo kwa wanufaika, kwa kuzingatia maoni ya wadau wake wakiwamo wanachama, watoa huduma na waajiri.

Kuhusu madai ya kuwasilisha Muswada bungeni kulazimisha mashirika makubwa kujiunga na Mfuko huo, alisema sheria ya Mfuko inaelekeza watumishi wote wa umma, walio katika wizara, idara, taasisi na mashirika ya umma, kujiunga kwa kuchangia asilimia tatu ya mshahara na mwajiri naye anachangia asilimia tatu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo