Lipumba ‘ampindua’ Maalim Seif


Celina Mathew

Ibrahim Lipumba
MWENYEKITI wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ametangaza rasmi kuwa nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama hicho ya Maalim Seif Sharrif Hamad itakaimiwa na Magdalena Sakaya kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana, wakati akitoa maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichofanyika Machi 25 na 26.

Profesa Lipumba alisema Baraza hilo limesikitishwa na kukasirishwa na vitendo vya Maalim kuhujumu chama na kupandikiza chuki, uhasidi na uhasama dhidi yake, hasa miongoni mwa wanachama wa CUF Zanzibar.

“Tangu Septemba mwaka jana, Katibu Mkuu hajafika ofisi kuu za chama amekaidi mwito wa Mwenyekiti wa kuja ofisi kuu kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.

“Baraza Kuu limeagiza kuwa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 toleo la 2014 ibara ya 93 (3) ambayo inaeleza Katibu Mkuu anapokuwa nje ya nchi au atakaposhindwa kufanya kazi zake kwa sababu yoyote ile, Naibu Katibu Mkuu anayemfuata kwa madaraka, atakaimu ukatibu mkuu hadi atakapokuwa tayari kuendelea na majukumu, iheshimiwe na kutekelezwa,” alisema.

Alisema Baraza limejiridhisha kuwa Katibu Mkuu ameshindwa kutimiza majukumu yake na kwa kuzingatia Katiba, Baraza linatangaza rasmi kuwa Sakaya ndiye anayemfuata Maalim kwa madaraka na atafanya kazi zote za Katibu Mkuu.

Aidha, aliziarifu ofisi za CUF za wilaya na asasi zote kuwa mawasiliano yote kuhusu masuala ya chama yawasilishwe kwa Sakaya katika ofisi za Buguruni, Dar es Salaam na kwamba zinazotolewa na Maalim zipuuzwe.

Ashangazwa

Wakati huo huo, alisema Baraza hilo linashangazwa na Maalim Seif kujenga urafiki na Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye akiwa ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa Serikali iliyotekeleza operesheni ya kusababisha mauaji ya wanachama wa CUF kwenye maandamano ya Januari 26 na 27, 2001.

“Katibu Mkuu anasahau mauaji hayo na anamfanya Sumaye  swahiba wake wa karibu na alitangaza hadharani kwamba kama kiongozi wa Chadema nia yake ni kuhakikisha Tanzania ina vyama viwili (CCM na Chadema), ni wazi kwamba lengo lao ni kuiua CUF kwa manufaa ya chama chake,” alisema.

Alimtaka Maalim kuacha mkakati wa kuiua CUF Bara ili kuistawisha Chadema kwa kisingizio cha Ukawa.

Aliongeza kuwa kwa sasa safari zote za chama zinaratibiwa na Sakaya au wasaidizi wake na kumwagiza Maalim asifanye ziara yoyote ya chama Bara kwa kuwa Baraza limejiridhisha kwamba kwa sasa mpango wake ni kukihujumu kwa kushirikiana na viongozi wa nje.

Kuhojiwa

Profesa Lipumba aliongeza kuwa Baraza limeteua wajumbe watatu wa Kamati ya Maadili, ambao ni Mashaka Njole, Hamis Hassan na Rukhia Kassim ambao wataungana na waliotajwa kwenye Katiba ibara ya 99 kifungu cha (2)(i-v) ambayo itawaita Maalim na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor Mazrui na kuwahoji.

Alisema Maalim Seif atahojiwa kwa kushindwa kutimiza majukumu yake kwa kutofika kwenye ofisi za chama hicho na kukaidi mwito wa Profesa Lipumba ambaye ndiyo Mwenyekiti ili kupewa maelekezo ya kuandaa vikao vya chama.

Pia Mazrui ataitwa kuhojiwa kwa kutoa kauli za dharau na kejeli dhidi ya Mwenyekiti na wabunge wawili waliofanya hujuma kwa kuacha kumnadi mgombea udiwani wa CUF wa kata ya Kiwanja cha Ndege, Morogoro na badala yake wakamnadi mgombea wa Chadema.

Alisema mbunge mwingine ni aliyemshawishi mgombea udiwani wa CUF kata ya Kiwani, Muleba kuhama chama na kugombea udiwani kupitia Chadema.

Wagombea EALA

Pia Baraza hilo lilipokea majina saba ya wanachama waliojitokeza kugombea ubunge wa Afrika Mashariki ambao ni Mneke Jaafar, Khalifa Khalifa, Zainabu Mndolwa, Dadi Hemed, Thomas Malima, Mohammed Mnyaa na Sonia Magogo.

Alisema Baraza lilizingatia kanuni za uchaguzi wa wabunge wa jumuiya hiyo na kuteua majina matatu ambayo walikubaliana mmoja awe mwanamke, mwingine atoke Zanzibar na aliyebaki atoke Bara.

Profesa Lipumba alisema baada ya majadiliano, Baraza Kuu liliteua wagombea watatu ambao ni Magogo, Mnyaa na Malima.

Bodi mpya

Aidha, Baraza liliteua wajumbe wa Bodi mpya ambao ni Peter Malebo, Abdul Magomba, Hajra Silia, Amina Thomas na Aziz Dagesh kutoka Bara na Salha Hilal, Asha Said, Suleiman Issa na Mussa Kombo kutoka Zanzibar.

Aliagiza Bodi kufuatilia fedha za ruzuku kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ili ipatikane na kuendeleza shughuli za ujenzi wa chama na kuhakikisha akaunti zote zilizositishwa na Maalim zinafunguliwa.

Pia kufuatilia kesi zilizofunguliwa kwa jina la chama kama zina tija kwa chama na kufuatilia hali ya miradi iliyoanzishwa na chama maeneo mbalimbali nchini na kuwasilisha taarifa zake kwenye kikao cha Bodi.

Nafasi wazi

Baraza hilo lilijaza nafasi zilizokuwa wazi kwa kutumia mapendekezo yaliyopelekwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa kuwapitisha Abeid Mlapakolo kutoka kanda ya Pwani kuwa mjumbe akichukua nafasi ya marehemu Ashura Mustapha.

Wengine ni Martha Haule kutoka Kanda ya Ziwa kuchukua nafasi ya Mkiwa Kimwanga aliyehama chama mwaka juzi, Dauda Hassan kutoka Kanda ya Kati kuchukua nafasi ya Chifu Lutalosa Yemba aliyevuliwa uanachama na Baraza.

Pia Juma Nindi kuchukua nafasi ya Lobora Ndarapoi aliyehama chama mwaka 2015 na Maisara Mshamu kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini anayechukua nafasi ya Mohammed Khalifa aliyehama chama mwaka juzi.

Wakurugenzi

Baraza lilithibitisha kwa kauli moja uteuzi wa Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Uchaguzi na Bunge ambaye pia anakaimu nafasi ya Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria, Nassor Seif, Naibu Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Uchaguzi na Bunge Mneke Jaafar, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma, Abdul Kambaya.

Wengine ni Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi, Thomas Malima, Naibu Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Maftaha Nachuma.

Aidha, Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Khalifa Khalifa, Naibu Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, Masoud Mhina na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria, Zainab Mndolwa.

“Wajumbe hawa ndio wanaounda Kamati ya Utendaji mpya itakayofanya kazi za chama ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Kaimu Katibu Mkuu Sakaya,” alisema Profesa Lipumba.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo