Amri ya JPM yakimbiza Sh. trilioni 2—Zitto


Suleiman Msuya

Zitto Kabwe
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema amri ya Rais John Magufuli kuzuia mchanga wa dhahabu kutoka katika migodi mbalimbali kusafirishwa kwenda nje umelipotezea Taifa Sh. trilioni 1.8 ambazo zingelipwa kama kodi ya ongezeko la mtaji.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo alisema hayo mkoani Arusha katika kongamano la maadhimisho ya miaka 50 ya Azimio la Arusha juzi.

Alisema ni jukumu la viongozi kuzingatia umakini katika utoaji kauli mbalimbali ili kuepusha migongano au hasara kwa Taifa.

“Juzi katika mkutano wetu pamoja na kuzungumzia Azimio la Arusha nilizungumzia suala la umakini wa viongozi katika kauli zao kiongozi lazima ujue unatoa kauli gani wakati gani,” alisema.

Kupitia waraka alioutuma kwa vyombo vya habari, Zitto alisema aliwaeleza wanachama na wageni wengine katika mkutano wa ACT Wazalendo kuwa amri aliyoitoa Rais Magufuli kuzuia usafirishaji wa mchanga wa dhahabu imesababisha Taifa kupoteza dola za Marekani milioni 880.
Alifafanua kwamba fedha hizo zingelipwa kama kodi ya ongezeko la mtaji kutokana na mauzo ya Kampuni ya Madini ya Acacia yaliyokwishaanza lakini yamevunjika baada ya amri ya Rais Magufuli. 

Kiongozi huyo alisema hivi sasa Tanzania ina sheria ya kutoza asilimia 20 ya thamani ya mauzo iwapo kampuni zinauziana hisa.

Alisema sheria hiyo ilitungwa mwaka 2012 ili kukabili wawekezaji waliokuwa wanauziana kampuni bila Tanzania kupata lolote.

“Tanzania imeshafaidika na kodi hiyo kwa mauzo mbalimbali ambayo yamekwisha fanyika kwenye sekta mbalimbali,” alisema. 

Mbunge huyo alisema wakati Rais anatoa amri kuzuia  mchanga wa madini kusafirishwa nje ya nchi, kulikuwa na mazungumzo yakiendelea kati ya Kampuni ya Acacia  ( yenye migodi inayozalisha nchini Tanzania ambazo - Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara) na kampuni nyengine ya nchini Canada ambapo ingenunuliwa kwa dola za Marekani bilioni 4.4 .

Mbunge huyo wa Kigoma Mjini alisema tafiti zinaonyesha kuwa gharama ya kujenga mtambo wa kuchenjua dhahabu nchini ni dola za Marekani milioni 800 hivyo mapato ambayo yangepatikana kutokana na kodi ya mauzo ya Acacia yangewezesha nchi kujenga kiwanda hicho na kufikia lengo la Rais la kuwezesha uchenjuaji wa mchanga hapa hapa nchini.

“Rais angetulia, angeweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja, kiwanda cha kuchenjua kingejengwa nchini na mchanga usingesafirishwa tena kwenda China na Japan,” alisema Zitto. 

Alibainisha kuwa Tanzania haina mchanga wa kutosha wa kushibisha mtambo wa uchenjuaji madini kwa mujibu wa teknolojia ya sasa.

Alisema fedha hizo zingiweza kutumika katika miradi ya maendeleo mbalimbali kama ujenzi wa reli ya kisasa ambapo Serikali imeshaingia mikataba na kampuni mbalimbali hivyo kuepuka kukopa. 

Aidha, alisema pia fedha hizo zingesaidia ujenzi wa vyuo vya veta kila wilaya na kila kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na chenji ingebaki.

“Tanzania inahitaji Sh. bilioni 750 kujenga vyuo vya Veta kila wilaya, miji, manispaa na majiji yote nchini,” alisema.


Alisema: “Binafsi naunga mkono kuwa ni lazima tuchenjue dhahabu hapa hapa nchini badala ya kupeleka mchanga Japan na China lakini ni muhimu uamuzi huo uwe na ushahidi wa kisayansi badala ya matamko yenye madhara.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo