Makonda adaiwa kuivuruga Dola



*Matendo, kauli zake zasababisha mkanganyiko
*Sifa anazopewa na Rais sasa zaibua mjadala mkali

Waandishi Wetu

Paul Makonda
NI wazi kuwa tuhuma zinazomkabili Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda zinaigonganisha mihimili ya Dola na kuzua sintofahamu miongoni mwa wateule wa Rais John Magufuli.

Tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda ametoa kauli tata akituhumiwa katika mambo tofauti na kufanya vitendo vilivyozua mjadala jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya siasa waliozungumza na gazeti hili, wametaja athari zinazoweza kutokea iwapo mamlaka hazitachukua hatua.

“Inawezekana Rais John Magufuli ana vyanzo vyake vinavyompa habari hivyo anajua utendaji na hatua zote zinazofanywa na mteule wake huyo.

Athari zinaweza kutokea iwapo Rais atashindwa kuchukua hatua za kinidhamu, maana wananchi wanajua na kuona na wanasubiri hatua zichukuliwe,” alisema Hamad Salim, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT).

Ijumaa iliyopita, Makonda anayetajwa kuivuruga mihimili mitatu ya Dola; Serikali, Bunge na Mahakama aliingia studio za Clouds TV usiku akiwa na askari na silaha za moto, tukio ambalo lilithibitishwa na Mkurugenzi wa Vipindi na Uendeshaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba.

Ruge alisema Makonda aliingia studio kuchukua kinguvu sehemu ya kipindi cha Shilawadu kilichokuwa kimezuiwa kurushwa kutokana na kutokidhi matakwa ya kitaaluma, kikimhusisha mwanamke anayedaiwa kuwa mzazi mwenzake na hasimu wa Makonda, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Makonda pia anahusishwa na mtu anayeitwa Daudi Bashite aliyesoma Shule ya Msingi Koromije na Sekondari ya Pamba na kumaliza kidato cha nne na kupata daraja la sifuri kabla ya kughushi cheti na kuendelea na elimu ya juu.

Mkuu huyo wa mkoa pia anatakiwa kwenda kujieleza kwenye Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge, akituhumiwa kukashifu wabunge kuwa wakati mwingine hukosa cha kuzungumza na ndiyo maana husinzia bungeni.

Tukio la juzi la Clouds lilimfanya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuunda kamati ya kulichunguza na kutoa majibu ndani ya saa 24, huku wadau wa habari wakitoa kauli za kupinga kuvamiwa kwa ofisi za Clouds kwa maelezo kuwa ni kuminya uhuru wa vyombo vya habari.

Licha ya tuhuma hizo, Rais Magufuli juzi alitumia ufunguzi wa mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara za Sam Nujoma na Morogoro jijini hapa, kumtaka mkuu huyo wa mkoa kuchapa kazi na kutosikiliza habari alizoziita kuwa ni za mtandaoni na udaku.

Wachambuzi Katika ufafanuzi zaidi, Hamad alisema: “Kitendo cha kuvamia chombo cha habari si cha kiungwana, nafikiri Rais alipaswa kutumia busara zaidi katika kulizungumzia hili, kwa sababu kama mteule wake anaandamwa na kashfa kila kukicha na yeye hachukui hatua, basi wananchi wanaweza kuuchoka utawala wake.”

Aliongeza: “Kumsifia sana kunaweza kuzaa tafsiri mbaya kwa wananchi, wengine wanaweza kudhani kuna mkono wake katika hili na ndiyo maana inampa ugumu kuchukua hatua. Kimsingi Rais ataharibu taswira nzuri ambayo alishaanza kujijengea.”

Alibainisha kuwa kauli ya Rais Magufuli kuwa watu wenye akili ndogo hujikita katika kuzungumzia maisha binafsi ya watu, ni sawa na kutukana wananchi kwa maelezo kuwa wananchi kuhoji cheti cha Makonda ni haki yao.

“Wapo ndugu na jamaa zao ambao wamepoteza ajira kwa kughushi vyeti, sasa wanaposikia mkuu wao wa mkoa ana tuhuma kama hizo, lazima wahoji. Ni kama Nape anataka kuchukua hatua lakini Rais anaonekana kuwa na imani na Makonda,” alisema Hamad.

“Mfano matamko yanayotolewa na Makonda… anaonekana kuwa juu ya sheria na hakuna wa kumfanya lolote. Hii inachafua sura ya Serikali kwa sababu viongozi wanaonekana kuvunja sheria na bado Rais anawasifia.”

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema mambo yanayofanywa na Makonda ni kinyume na maadili na mwongozo wa Sheria ya Utumishi wa Umma.

“Ni kuishushia heshima Serikali na kuwafanya wananchi kupata shaka nayo. Rais kumsifia Makonda licha ya kuandamwa na tuhuma kibao ukiwamo uvamizi ni sawa na kuhalalisha tabia hiyo kwa viongozi wengine wa Serikali ambao sasa wanaweza kufanya kama alivyofanya Makonda,” alisema Dk Kyauke.

Hata hivyo, mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk Benson Bana alihoji sababu za kuibuka kwa tuhuma za Makonda sasa, si wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

“Makonda amekuwa mfano wa kuigwa kwa wakuu wengine wa mkoa kutokana na ufanisi wake wa kazi. Inawezekana yanayosemwa kuhusu yeye ni kutokana na vita aliyoianzisha dhidi ya dawa za kulevya,” alisema.

Kauli ya Dk Bana ilipingwa na Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) na kubainisha kuwa Rais kumkingia kifua Makonda kutaifanya nchi kuingia kwenye mgogoro na mashirika ya kimataifa kwa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.

“Kauli ya Magufuli dhidi ya Makonda jana (juzi) ni mbaya kwa Taifa kwa sababu inachukua sura ya Rais na kufuta mazuri yote aliyofanya hadi sasa. Makonda mwenyewe atashusha heshima yake na kuonekana kila analolifanya lina baraka kutoka Mamlaka ya juu,” alisema Sakaya.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo