Sinema ya Makonda yafika patamu


WAANDISHI WETU

Paul Makonda
ALIKOROGA, alinywa. Ndivyo unavyoweza kufananisha kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia Kituo cha Televisheni cha Clouds juzi na kulazimisha kirushwe kipindi cha kumchafua Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufunuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Sinema hiyo ilishika kasi baada ya hivi karibuni Gwajima kudai kuwa Makonda anatumia jina ambalo sio lake. Anajiita Paul Makonda wakati jina lake halisi ni Daud Albert Bashite.

Kabla ya kuvamia kituo hicho akiwa na askari kadhaa, wiki tatu zilizopita, Makonda alidaiwa kutuma watu kijijini kwake kwa lengo la kuandika taarifa za kumsafisha na kusambaza kwenye vyombo vya habari.

Alivyovamia TV
Makonda alidaiwa kuvamia kituo hicho cha televisheni cha Clouds na kulazimisha waongoza kipindi cha Shilawadu kuonesha video za mwanamke ambaye inadaiwa kuwa amezaa na Askofu Gwajima.

Kitendo cha Makonda kwenda Clouds kinaelezwa kuwa kimetokana na kituo hicho cha televisheni kutorusha kipindi hicho ambacho alikipeleka siku kadhaa nyuma.

Video iliyorushwa kwenye mitandao jana zilimwonyesha Makonda akiwa na askari wanne; wawili wakiwa wamevalia kijeshi wakiwa na bunduki na wengine sare ya Polisi wakiingia kwenye kituo hicho cha televisheni wakidaiwa kulazimisha CD iliyokuwa na tukio la mwanamke huyo irushwe.

Kauli ya Askofu Gwajima
Akizungumza na waumini wa Kanisa lake Askofu Gwajima alisema kinachoendelea ni vichekesho kwa kuwa matendo ya Makonda yanadhalilisha Serikali.

Gwajima alisema anachoona ni kuwa Serikali inapambana na yeye jambo ambalo si sahihi kwani yeye hoja yake ilikuwa imejikita kwa Makonda pekee kwa kughushi vyeti.

Alisema kilichotokea kwa yeye kuhusishwa na kuzaa na mwanamke huyo aliyemtambulisha kuwa ni mke wa mtu aliyetambulika kwa jina la Said Kipingu, ni mipango ya Bashite (Makonda) kufikiri kuwa angejibu mapigo.

Askofu Gwajima alisema kipindi hicho kilichoandaliwa na waandaaji wa Shilawadu kilipangwa kurushwe Ijumaa ila ilishindikana kutokana na maadili ya taaluma ya habari. “Bashite alivyoona kipindi hakirushwi, alilazimika kwenda Clouds TV kulazimisha kipindi kiendelee, lakini ilishindikana na ndipo waliamua kurusha kwenye mitandao ya kijamii,” alisema.

Gwajima alisema jitihada zinazofanywa na wabaya wake zinaweza kuua mwili tu na siyo roho yake, hivyo hawataweza kufanikiwa.

Alisema atahakikisha popote ambapo kumepinda kunanyooka ili kurejesha heshima ya nchi na wananchi na kwamba hatokubali kuwa sehemu ya watu waoga.

“Unaliamsha dude, unawasha moto bila kuwa na kikosi cha zima moto hivyo sipo tayari kuona watu wakipindisha ukweli nitanyoosha,” alisema.

Mbunge Kingu naye atoa neno
Mbunge wa Ikungi, Elibariki Kingu ameeleza kuwa yupo tayari kufukuzwa CCM iwapo hakuna hatua ambazo zitachukuliwa dhidi ya Makonda kwa tukio hilo.

Mbunge huyo aliandika katika mitandao ya kijamii akiponda mambo yanayofanywa na Makonda kwa maelezo kuwa yanamdhalilisha Rais Magufuli.

Kingu alisema yeye atakuwa wa kwanza kufukuzwa CCM kama mamlaka husika zitafumbia macho kitendo cha Makonda kuvamia kituo hicho cha runinga. Alisema kitendo alichofanya Makonda hakikubaliki isipokuwa katika nchi za Somalia, Sudani Kusini, Afghanistani na nchi nyingine zenye vita.

“Haiwezekani Rais wetu aonekane wa ajabu kila kona kwa matendo ya mtu huyu. Wana CCM kwenye hili ukimya wetu hautusaidii…, naomba niwe wa kwanza kufukuzwa CCM kwa kumpinga RC Makonda,” alisema Kingu.

Alisema kinachoonekana ni Makonda kulewa madaraka hali ambayo inadhalilisha vijana ambao wamepewa nafasi ya kuongoza nchi katika ngazi mbalimbali.

Alisema akiwa kijana hatovumilia mambo ambayo hayana tija kwa chama na kwamba hata Rais hajawaambia wasikemee mapungufu yanayotokea.  “Ametuchafua sana hivi RC unatembea na askari zaidi ya sita unaenda kuvamia chombo cha habari hii ni fedheha na mimi siwezi kuvumilia huu ndio msimamo wangu,” alisema.

Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe, alitaka vyombo vya ulinzi kulinda heshima yake kwani katika siku za hivi karibuni vimekuwa vikitumika vibaya.

Alisema hayo kupitia mtandao wake wa Twita. “Nimeona Dodoma kwangu binafsi na hilo la Clouds lazima lilaaniwe,” alisema.

Mkurugenzi Clouds atoa ya moyoni
Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba aliahidi kutoa ufafanuzi wa suala hilo baadaye kwa kuwa wafanyakazi wameshikwa na bumbuwazi kufuatia kitendo hicho.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa ‘twitter’ akieleza kuwa leo atafika katika studio za Clouds kufuatilia kilichotokea jana akiwataka wanahabari kuwa watulivu.

JAMBOLEO ilijitahidi kumtafuta Makonda kupitia simu zake mbili za Airtel na Tigo lakini zote ziliita bila kupokelewa.

Sakata la Makonda limeweza kuteka mitandao ya kijamii kwa takribani mwezi sasa hata pale ambapo limetokea tukio kubwa limekuwa likidumu kwa saa na hoja ya usahihi wa vyeti vya Makonda ukiwa ni ndio mjadala mkubwa bila kupatiwa majibu.

Wakati Watanzania wakitaka kupata jibu la uhalali wa vyeti vya Makonda Rais John Magufuli ambaye aliingia madarakani na kuanza kazi ya kuondoa wafanyakazi hewa na wenye vyeti vya kughushi amekuwa kimya katika hili hali ambayo inazidi kuibua maswali mengi kwa jamii.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo