Nape aunda kamati kumchunguza Makonda


Hussein Ndumbikile

Nape Nnauye
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ameunda kamati ya watu watano kuchunguza kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda cha kuvamia ofisi za Clouds Media Group (CMG) Ijumaa usiku.

Kamati hiyo imeundwa baada ya Waziri Nape kufanya ziara jana CMG na kuzungumza na uongozi wa chombo hicho cha habari baada ya Mkuu wa Mkoa huyo kufanya kitendo hicho akiwa na askari wenye silaha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo, Zawadi Msalla, Kamati hiyo itaongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO, Dk Hassan Abbas.

Wajumbe wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, Mhariri wa Nipashe, Jesse Kwayu, Nengida Johannes wa Wapo Radio na Mabel Masasi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Taarifa hiyo ilisema Kamati hiyo itafanya uchunguzi wa kina ili kujiridhisha kutoka pande zote ambapo Wizara itasema hatua itakazochukua.

Wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa huyo kupitia picha za mitandao ya kijamii, alionekana akivamia ofisi za kituo hicho cha habari akiwa na askari hali iliyoleta sintofahamu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo