…‘Aning’inizwa’ kitanzini na wanahabari


Waandishi Wetu

Paul Makonda
TANGU gazeti hili lilipochapisha kwa mara ya kwanza tuhuma za utata wa elimu ya Paul Makonda, zimepita siku 32 za mjadala mkubwa kuhusu jina la Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mjadala huo uliotokana na kauli na matendo yake tangu kuibuliwa kwa tuhuma hizo na zingine nyingi, ulifikia ukomo jana baada ya vyombo vya habari kutangaza marufuku ya kutochapisha au kutangaza habari zinazomhusisha kiongozi huyo wa mkoa.

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Klabu ya Waandishi wa Habari Dar es Salaam jana walikutana na waandishi wa habari na kutoa tamko hilo ikiwa ni siku chache tangu Makonda kuvamia ofisi ya kituo cha Televisheni chaClouds Media, akiwa na askari wenye silaha za moto.

“Makonda alitoa amri ya kulazimisha kurushwa hewani kwa kipindi cha televisheni, kutumia nguvu na kupora kipindi mali ya Clouds,” alisema Neville Meena, Katibu wa TEF.

Ilivyoanza

Februari 21, Makonda wakati akikabidhiwa eneo la ekari 1,500 lililotolewa kwa uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na kampuni ya Azimio Estate kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo, aliulizwa swali na mwandishi wa gazeti hili kuhusu elimu yake, badala ya kujibu alitumia simu ya mwandishi huyo kuzungumza na Mhariri wa Habari wa JAMBO LEO na kumporomoshea matusi.

Licha ya kutoa lugha chafu, Makonda alisema habari hiyo haiwezi kumwondoa mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji katika tuhuma za dawa za kulevya.

Kuanzia hapo, vyombo vya habari vilifuatilia tuhuma hizo kwa kusaka ukweli katika shule anazodaiwa kusoma huku mjadala huo ukikolezwa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Ilivyotokea

Siku sita baada ya Makonda kukabidhiwa eneo hilo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alizuia ekari hizo za ardhi kwa maelezo kuwa ni mali ya Serikali.

Akizungumza na wanahabari, Lukuvi alisema Makonda alidanganywa kuhusu ekari hizo zilizoko eneo la Kisarawe 11 wilaya ya Kigamboni kwa maelezo kuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Mohamed Iqbal alishindwa kesi mahakamani ambayo ilifunguliwa na wananchi.

Kuhusu elimu, Makonda anahusishwa na mtu anayeitwa Daudi Bashite aliyesoma shule ya msingi Koromije na sekondari ya Pamba na kumaliza kidato cha nne kwa kupata daraja sifuri kabla ya kughushi cheti na kuendelea na elimu ya juu.

Sakata hilo la kughushi cheti cha kidato cha nne liliandikwa na magazeti kadhaa nchini, huku likishika kasi kwenye mitandao ya kijamii na kila Mkuu wa Mkoa alipoulizwa, alikosa majibu.

Wakati hayo yakiendelea, Makonda anatakiwa kwenda kujieleza katika Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge akituhumiwa kukashifu wabunge kuwa wakati mwingine hukosa cha kuzungumza na ndiyo maana husinzia bungeni.

Mjadala zaidi uliibuka baada ya Makonda kwenda Clouds akiwa na askari wenye silaha za moto, tukio ambalo lilithibitishwa na Mkurugenzi wa Vipindi na Uendeshaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba.

Ruge alisema Makonda aliingia studio kuchukua kinguvu sehemu ya kipindi cha Shilawadu kilichokuwa akimezuiwa kurushwa kutokana na kutokidhi matakwa ya kitaaluma, kikimhusisha mwanamke anayedaiwa kuwa kuwa na uhusiano na Askofu Gwajima.

Msumari

“Tunalaani vikali vitendo hivyo vya Makonda, kwa pamoja tumeazimia kutoandika au kutangaza habari zote zinazomhusisha katika vyombo vyetu vya habari,” alisema Meena.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanamtangaza Makonda kuwa adui wa uhuru wa vyombo vya habari huku akibainisha atakayeshirikiana naye kitakachompata hawatamtetea.

Meena alifafanua kuwa utekelezaji wa agizo hilo unaanza mara moja kwani walishakubaliana na Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Tanzania (UTPC) kupitia Rais wake, Deo Nsokolo.

“Kuanzia sasa mkutano na waandishi wa habari akatafute vyombo vya habari vya nje na mwandishi wa habari atakayekwenda huko litakalompata hakuna mtu atakayesimama kumtetea,” alisema.

“Ukienda huko ukafanyiwa jambo lolote ukatukanwa, hatutahusika maana sisi klabu za waandishi wa habari tunajivua lawama kwa atakayekwenda kwenye mkutano wa Makonda atakachokufanya ni juu yako.”

Alisema endapo ikitokea Makonda ameitwa bungeni, wahariri wataamua nini la kufanya kuhusu kuripoti habari hizo.

Alisema hawawezi kuweka mipaka kwa asilimia 100 ya kutoandika habari zake, bali kutoandika habari ambazo alikuwa akizitumia kama ngazi na kumpa sauti.

“Kama kutakuwa na kiongozi ataambatana na Makonda kwenye jambo lenye maslahi ya wananchi wa mkoa, waandishi watatangaza habari ya kiongozi aliyeambatana naye na si Makonda,” alisema Meena.

Alisema waandishi wanatakiwa kushiriki matukio anayoshiriki na si kumtangaza kwenye televisheni, redio na magazeti.

“Tungependa kutoa mwito hata kwa watu ambao wanafanya kazi mitandaoni (online), wajue kilichowapata Clouds nao kinaweza kuwapata,” alisisitiza.

Meena alifafanua kuwa utaratibu huo utaendelea hadi hapo utakapotangazwa au kuamriwa vinginevyo huku akibainisha kuwa malalamiko ya Makonda si ya leo kwani amekuwa akitoa kauli za kejeli na kudhalilisha waandishi wa habari katika vikao vyake mbalimbali.

Alitoa wito kwa vyombo vya habari nje ya mkoa kutompa sauti kwani kitu kitakachowakuta hakuna atakayehusika kwa lolote.

Meena alifafanua kuwa Rais John Magufuli alimwambia Makonda achape kazi, alimaanisha si kwenda kituo cha televisheni na polisi wenye silaha usiku.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo