Serikali kujenga meli kubwa Kanda ya Ziwa


Mwandishi Wetu

SERIKALI imesema ipo katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za ujenzi wa meli mpya kubwa ya kisasa itakayokuwa na uwezo wa kuchukua tani 300 za mizigo, magari 25 na madaraja matatu kwa ajili ya sehemu ya kukaa abiria.

Aidha, imesema haitavumilia wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga katika hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua Bandari ya Bukoba, mkoani Kagera, Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema utekelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na kukosa sifa kwa makandarasi wawili waliojitokeza mwanzoni kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa ujenzi.

“Nataka kujenga meli ya kisasa ili kuweza kufupisha safari kutoka masaa 10 hadi matano kutoka Bukoba hadi Mwanza, hivyo kufanya usafiri wa majini kuwa wa kuaminika na salama”, alisema Mbarawa.

Aidha, alifafanua kuwa kutokana na utendaji mbovu wa bandari hiyo anatarajia kuleta wafanyakazi makini kwa ajili ya kupitia taarifa za kifedha na usafirishwaji wa mizigo bandarini hapo.

Meneja wa Mamlaka ya Bandari Kanda ya Ziwa, Abel Moyo aliiomba Serikali kufanya ukarabati wa meli nchini hasa zilizopo Kanda ya Ziwa ili kuweza kuondoa adha wanazozipata wakazi wa mikoa hiyo.

Katika hatua nyingine, Mbarawa amekagua Shirika la Posta mkoani humo na kuahidi kupeleka wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kukagua na kujiridhisha juu ya mapato na matumizi ili kubaini ubadhilifu unaofanywa na watendaji.

“Tunataka Posta iwe safi na kupunguza changamoto zinazoikabili kwani ni Shirika kubwa na lenye rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuinua mapato ya shirika”, alisisitiza.

Aidha, Mbarawa ameagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa katika utengenezaji wa magari yanayokuja kupata huduma katika karakana yao.

Kwa upande wake, Meneja wa Temesa Mhandisi Zephrine Bahyona amemuomba waziri kusaidia kusisitiza taasisi za Serikali kupeleka magari yao kwenye karakana zao na kulipa madeni kwa wakati ili kupunguzia Wakala huo mzigo wa madeni kutoka katika taasisi hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Karagwe, mkoani Kagera baada ya kukagua barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Mbarawa amewataka wananchi kuacha dhana ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.

"Najua bado kuna watu wanaendelea kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema kuwa Serikali itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja sheria", amesema Profesa Mbarawa.

Kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Mbarawa amekipongeza Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), kwa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa kuzingatia viwango.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo