Mwenyekiti CCK ahadharisha kuhusu Taifa


Suleiman Msuya

Constatine Akitanda
MWENYEKITI wa Chama Cha Kijamii (CCK), Constatine Akitanda, amesema iwapo hakutakuwa na hatua zitakazochukuliwa kuhusu kauli na uendeshaji wa nchi, Taifa litakwama.

Akitanda alisema hayo jana wakati akizungumza na JAMBOLEO Dar es Salaam akibainisha kuwa kila mtu ameweka kichwa chini na kushindwa kutoa ushauri kwa watawala.

Alisema iwapo nchi itaendeshwa bila ushauriano, kusikilizana na kuchukuliana hatua, ni dhahiri nchi inaweza kukwama kwa siku za karibuni.

Mwenyekiti huyo alisema kauli za kiongozi wa nchi kuwa hakuna mtu aliyemchukulia fomu ya kugombea urais, anaamini haina afya kwa jamii hata Taifa la Tanzania.

Alisema ni vema Katiba, sheria na kanuni za uongozi zikazingatiwa ili kulinusuru Taifa na iwapo kikombe cha uovu kikijaa ni vigumu nchi kutawalika.

“Nchi hii ina watu wenye akili wanaopaswa kusikilizwa, lakini kwa sababu hatusikilizwi ndiyo maana tumenyamaza ila tunafuatilia kila jambo,” alisema.

Akitanda alisema Tanzania ni ya Watanzania wote, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kusikilizwa na isionekane kuwa mtu mmoja au kundi fulani ndilo litavusha nchi.

Alisema kila kona ya nchi Watanzania wanalia kutokana na aina ya utawala ambao alidai kuwa una vimelea vya ubabe jambo ambalo si sahihi.

Mwenyekiti huyo alisema CCK inatafakari na kukusanya kila jambo ambalo linaendelea, ili kujiridhisha na wakati ukifika watatoa taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo.

Alitoa mwito kwa umma kuendelea kuvumilia na kuipigania Tanzania yao, ili kufanikisha dhamira ya maendeleo ambayo imekuwa ikiimbwa na Rais John Magufuli.

Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahim Dovutwa alisema ili kuifanya nchi iendeshwe kwa misingi ya kidemokrasia ni vema Katiba ya mwaka 1977 iangaliwe upya kwa maslahi ya Taifa.

“Katiba ya mwaka 1977 ibara ya 37 inasema Rais halazimishwi kupokea ushauri wa mtu yeyote, hivyo ni lazima Katiba iangaliwe upya kwani inampa madaraka makubwa Rais,” alisema.

Dovutwa alisema mikakati yao ni kuhakikisha Katiba inatambua mgombea binafsi, uhuru wa tume ya uchaguzi, rais apingwe mahakamani, mahitaji ya kisheria ya vyama vya siasa na rais apate zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Alisema watu wamesahau katika tawala zote zilizopita changamoto ni lazima ziwepo kutokana na upya wa uongozi na malengo ambayo kiongozi amejiwekea.

“Mwinyi (Rais Ali Hassan), Mkapa (Rais Benjamin) na Kikwete (Rais Jakaya) walikutana na changamoto hizo katika awamu zao za kwanza hivyo ni vema wananchi wakazoea ila baadaye watafaidika,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo