Bunge laagiza SUA kufufua miradi ya ANC



Mwandishi Wetu 
                       
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imekiagiza Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kutafuta fedha kwa ajili ya kuiendeleza miradi yote iliyorithiwa na chuo hicho kutoka Chama cha Ukombozi wa Afrika ya Kusini (ANC).

PAC ilitoa agizo hilo jana wakati ilipotembelea chuo hicho na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na chuo ikiwemo hiyo iliyoachwa na chama cha ANC neo la Mazimbu mkoani Morogoro.

Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na shamba la nguruwe, shamba la kufugia ng'ombe, majengo, mashamba na vinu vya kuhifadhia nafaka.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Ujumbe wa Kamati hiyo, Shally Raymond alisema uongozi wa SUA, lazima uhakikishe miradi hiyo inafanya kazi ili iweze kuingiza mapato ya chuo, pia kuwasaidia Watanzania kwa ujumla.

"Miradi hii ni hazina kubwa tuliyoachiwa na ya gharama kubwa, tujitahidi tutafute fedha ili tuifufue iweze kufanya kazi kulingana na uwezo wake," alisema.

Alisema kwa sasa miradi hiyo inazalisha chini ya kiwango na kwamba SUA kinatakiwa kutafuta fedha ili kukarabati baadhi ya miundombinu pamoja na kupata mitaji ya kuendeleza miradi.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Gerald Monela alisema suala la kutoendeleza miradi hiyo ipasavyo limekuwa likiwaumiza viongozi wa SUA na limekuwa likijadiliwa mara kwa mara katika vikao vya Baraza la Chuo hicho.

"Tatizo kubwa ni ukosefu wa fedha kwa ajili ya mtaji na kukarabati baadhi ya mitambo ikiwemo mtambo mkubwa wa kuzalisha chakula cha mifugo, tumekuwa tukifanya michakato mbalimbali ya kuomba mikopo benki lakini tunakwama kutokana na kukosa dhamana kutoka Serikalini," alisema.

Alisema kwa sasa chuo hicho kimeanzisha kampuni itakayosimamia miradi yote ya chuo ikiwemo miradi ya ANC na kwamba kwa sasa kipo katika mchakato wa kumpata Meneja wa Kampuni hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo