Wabunge waponda bajeti ya trilioni 32/-


*Walaumu iliyopita kushindwa kufikiwa kikamilifu
*Wasema ni kutokana na Serikali inavyojiendesha

Sharifa Marira, Dodoma

SERIKALI imewasilisha Sura ya Bajeti yake ya mwaka 2017/18 ikionesha jumla ya Sh bilioni 31,699.7 zinatarajiwa kukusanywa huku wabunge wakiponda kuwa haitatekelezeka.

Wamesema hata bajeti iliyopita imeonekana kukwama kutokana na namna Serikali inavyojiendesha.

Akiwasilisha sura hiyo jana kwenye ukumbi wa Bunge mjini hapa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema fedha hizo zinatarajiwa kutoka vyanzo mbalimbali Sh bilioni 17,106.3 huku za kodi zikiwa ni Sh bilioni 2,183.4.

Alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh bilioni 3,971.1 ambayo ni asilimia 12.6 ya bajeti yote, ambapo Serikali inatarajia kukopa Sh bilioni 6,156.7 kutoka soko la ndani.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliponda Serikali kuongeza bajeti hadi zaidi ya Sh trilioni 31 wakati bajeti iliyopita iliyokuwa Sh trilioni 29 ilishindwa kufikiwa kutokana na wadau wa maendeleo kushindwa kuchangia.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (Act -Wazalendo) alisema katika taarifa iliyowasilishwa na Dk Mpango, hadi Februari mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia Sh bilioni 15,372.4 sawa na asilimia 79 ya lengo la kipindi hicho.

Alisema hali hiyo ilitokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kukosekana kwa mikopo yenye masharti nafuu, jambo alilosema lilitokana na utendaji wa Serikali.

"Misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ilikuwa ni Sh bilioni 1,253.6 pekee na sababu ya hali hiyo ni wadau kukosa imani na Serikali kwa matamko yake na kutoheshimu mikataba iliyowekwa na Serikali zilizopita," alisema Zitto.

Alisema bajeti hiyo si halisia na jambo ambalo haliwezekani kutekelezwa, ikiwa ya mwaka 2016/17 Serikali ilishindwa kufikisha Sh trilioni 29 ya mwaka unaomalizika.

“Hiyo ya Sh trilioni 31 itafikiwa lini?  Hadi sasa ni asilimia 52 tu ya bajeti nzima ndiyo ilipatikana nayo haina uhalisia wowote ni ya maandishi tu.

“Hata katika miradi ya maendeleo ambayo inadaiwa kutekelezwa kwa asilimia 35 haijakidhi haja ya maisha ya Watanzania, kwani miradi iliyotekelezeka ni ununuzi wa ndege na ujenzi wa reli pekee, wananchi hawana maji, barabara, umeme na huduma bora za afya," alisema na kuongeza:

"Kwa mara ya kwanza katika historia, Serikali imeshindwa kukopa Sh. trilioni tano, hii ni kutokana na kutoaminika kwake. Kumekuwa na utaratibu wa viongozi kutoa matamko yanayokinzana na mikataba ambayo yanawaogofya wahisani, hivyo kupandisha riba ili tushindwe kukopa."

Mbunge wa Siha, Dk Godwin Mollel (Chadema) alisema tatizo lililopo ni Serikali kuweka bajeti ya kufikirika wasiyo na uhakika wa kuipata na ndiyo sababu mara nyingi bajeti hazitekelezeki na wanashindwa kufikia malengo.

Alisema hakuna haja kwa Serikali kuongeza nakisi ya bajeti hadi Sh. trilioni 31 wakati katika bajeti inayoishia Juni wameshindwa kutimiza lengo la Sh trilioni 29 iliyokuwa imekusudiwa.

"Tusiwe tunaweka bajeti za kujidanganya, ili mambo yaende tuweke nakisi ambayo tuna uwezo wa kuifikia, ili mipango yetu iende sawa haiwezekani kila siku tunalalamika kwamba bajeti haijatekelezeka wakati tulikuja bungeni kuipitisha," alisema Mollel.

Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) alisema Serikali haijaeleza ni namna gani inakwenda kujenga uchumi wa viwanda, hakuna mahali sekta ya kilimo imeonekana kama ndio msingi mkuu wa viwanda, hivyo haelewi kama kuna viwanda bila kilimo.

Alisema katika nakisi hii ya bajeti inaonekana mapato ya ndani yanatakiwa kuongezeka kutoka Sh trilioni 15 hadi 19 jambo ambalo linampa shaka kwamba wananchi ndio watakaobebeshwa mzigo huo kwa kuongezwa kodi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo