CUF yapinga Tanzania kuipa Kenya madaktari


Mwinyimvua Nzukwi, Zanzibar

Julius Mtatiro
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimepinga hatua ya Serikali kuipa madaktari Kenya, badala yake kimeitaka kuhakikisha inaimarisha huduma za afya kwa wananchi wake.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya juzi Rais John Magufuli kutangaza kuipa Kenya madaktari 500 ili wakafanye kazi nchini humo baada ya madaktari wa nchi hiyo kugoma kwa muda mrefu sasa.

Akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza Kuu la CUF, Vuga mjini Zanzibar, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa muda wa chama hicho, Julius Mtatiro, alisema uamuzi wa Rais Magufuli haupaswi kutekelezwa kutokana na ukweli kwamba Tanzania ina mahitaji makubwa ya madaktari maeneo mbalimbali.

Mtatiro alisema hata kama ingelikuwa Tanzania imejitosheleza kwa wataalamu na uimara wa huduma za afya kwa watu wake, sasa si wakati mwafaka kupeleka madaktari nchini Kenya kutokana na kutetereka kwa uhusiano kati ya watumishi wa sekta hiyo na serikali ya nchi hiyo.

Mtatiro alieleza kuwa madaktari wa Kenya wamehoji sababu za serikali yao kuomba msaada wa madaktari 500 wakati huu wakati wao wamemaliza mgomo jambo linaloashiria kutokubalika kwa watendaji hao.

“Kila mmoja anajua lililokokea Kenya muda huu, madaktari wana mgogoro na serikali, vipi wanachukuliwa madaktari wetu kupelekwa huko bila ya kuhakikishiwa usalama wao?“ alihoji mwenyekiti huyo. Alieleza kuwa Tanzania ina upungufu wa madaktari 3,330 wanaoweza kuhudumia wananchi 8,000 hivyo bado Tanzania inahitaji kuajiri madaktari zaidi hasa katika maeneo ya mikoani.

“Inashangaza kuona wanawake wanakufa kwa ajili ya uzazi kutokana na kukosa madaktari au huduma stahiki za afya, lakini serikali inakubali kwa mbwembwe kupeleka madaktari katika nchi nyengine jambo ambalo kwa akili za kawaida tu halikubaliki”, alieleza Mtatiro.

Akizungumzia suala la uchumi alieleza kuwa umeendelea kudorora na wananchi kuwa na hali mbaya ya uchumi jamboa ambalo ni tofauti na katika awamu iliyopita.

“Katika awamu iliyopita serikali ilikuwa ikikusanya wastani wa shilingi bilioni 800 kwa mwezi lakini ilikuwa na uwezo kupeleka fedha katika maeneo ya utendaji” alieleza.

Alidai kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dk. John Mugufuli inakusanya Sh. trilioni 4.5 kwa mwezi, lakini inashindwa kupeleka fedha za kutosha katika sekta za huduma za jamii na kiasi kikubwa kuelekezwa kwenye ulipaji wa mishahara na madeni bila ya kuzingatia uwiano wa utoaji wa fedha za maendeleo na matumizi ya kawaida.

Mtatiro aliwataka wabunge wa chama chama hicho lazima wahakikishe wanafanya kazi ya kuibana serikali ili kuhakikisha inaimarisha uchumi kwa maslahi ya taifa.

Mkutano huo wa siku moja ulikutana mjini Unguja kujadili mambo mbali mbali yanayohusu chama hicho na taifa kwa ujumla kilihudhuriwa pia na katibu mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad sanjari na wajumbe wa baraza hilo waliotangazwa kuvuliwa nafasi zao na Mwenyekiti wa chama hicho anaetambuliwa na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa Profesa Ibrahim Haroun Lipumba.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo