Mbunge Chadema afariki dunia Uingereza


Emeresiana Athanas

Dk Elly Macha
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepata pigo baada ya Mbunge wake wa Viti Maalumu, Dk Elly Macha kufariki dunia kwa maradhi.

Taarifa ya kifo cha Mbunge hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene jana ilisema Dk Macha alifariki dunia jana kwenye hospitali ya New Cross Wolverhampton, Uingereza ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu.

"Kifo cha Mbunge wetu ni pigo kwetu, kwa Bunge na Taifa kwa ujumla, kwani wakati wa uhai wake alikuwa mchango mkubwa katika masuala ya kichama na bungeni pia alikuwa makini kupigania maslahi ya wananchi na hasa kundi la watu wenye ulemavu kwani alikuwa mwakilishi wao," alisema Makene.

Taarifa ya Spika wa Bunge iliyotolewa Dar es Salaam jana ilisema mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kurudishwa nchini inaendelea kwa kushirikiana na familia ya marehemu.

"Mipango ya kusafirisha mwili kuja nchini ikiwa na taratibu za mazishi zinafanyiwa kazi. Taarifa zaidi juu ya msiba huo zitaendelea kutolewa kwa kadri zitakavyopatikana," ilisema taarifa hiyo.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema Dk Macha alikuwa mmoja wa watu waliojitolea utaalamu na taaluma zao kukitumikia chama chao.

"Msiba huu ni moja ya mapigo makubwa kwetu sisi Chadema na Watanzania, kwani alitumia uzoefu wake kushauri chama katika masuala mbalimbali na kuwa mstari wa mbele katika haki kwa watu wenye ulemavu bungeni.

"Alifanya hivyo akiwa mwanachama wa kawaida hadi hapo alipogombea nafasi ya mjumbe wa Kamati Kuu na baadaye kuwa Mbunge wa Viti Maalumu," alisema Mbowe.

Alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa familia, ndugu, marafiki, viongozi wa chama, wanachama, na wote walioguswa na msiba huo.

Marehemu alichaguliwa mjumbe wa Kamati Kuu katika uchaguzi mkuu wa ndani ya chama mwaka 2014 na mwaka juzi alikuwa kati ya wagombea waliojitokeza kuwania uteuzi wa ubunge wa viti maalumu.  
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo